Home news MUDA WA HESABU KWA SASA, MUHIMU KUJIPANGA

MUDA WA HESABU KWA SASA, MUHIMU KUJIPANGA


 HESABU ambazo zinapigwa kwa sasa ni tofauti na zile za awali wakati Ligi Kuu Tanzania Bara inaanza. Kila timu inatazama namna ya kutimiza malengo ambayo imejiwekea.


Kazi kubwa ni kuona namna gani timu zinazopambana kubaki ndani ya ligi zitatimiza hesabu zao pamoja na zile zinazowania taji namna itakavyokuwa.


Ugumu haupo kwa timu pekee bali hata wachezaji nao wana kazi kubwa ya kufanya kutimiza majukumu yao pale ambapo wanapewa kazi ya kufanya.


Kwa sasa wakati ligi inakwenda ukingoni wapo wachezaji ambao watavuna kile ambacho walikipanda kwa kupata ofa nzuri na wengine kuongezewa mikataba ila yote itatokana na jitihada zao ambazo wamezifanya uwanjani.


Wale ambao wapo Ligi Daraja la Kwanza wanajua kile ambacho wamekivuna kwani tayari Geita na Mbeya Kwanza washapanda daraja. Kwa hatua ambayo wamefikia basi wanahitaji pongezi na kujipanga kwa umakini wakati ujao watakapokuwa wanashiriki ligi.


Ambazo zimepanda daraja zinapaswa zitambue kwamba ushindani ndani ya ligi ni mkubwa na kila timu inahitaji kupata ushindi ili kufikia malengo.


Zile ambazo zimeshindwa kupanda kwa msimu huu wakati wao upo msimu ujao zinapaswa kupambana kufikia malengo yao.


Kushindwa kwa sasa haina maana kwamba wao sio bora hapana ni hesabu tu zimewagomea  wanaweza kujipanga upya wakarudi wakaendelea na kasi yao ile walipokuwa wanaanza msimu.


Zitakazotoka Ligi Kuu Bara mpaka Ligi Daraja la Kwanza zina kazi ya kupanga mkakati upya ambao utawarejesha tena huku juu kwa kuwa inawezekana.


Kikubwa kinachohitajika ni maandalizi makini na kila mmoja kutimiza majukumu yake kwa wakati sahihi jambo hili litaongeza ushindani na kuleta matokeo mazuri.


Ila imekuwa bahati mbaya kila wakati timu nyingi kuanza kuonyesha ushindani kwenye mzunguko wa pili ambao ni wa lala salama jambo ambalo linawaongezea ugumu kufanya vizuri.


Zile ambazo zinapanda kutoka Ligi Daraja la Kwanza zina kazi kubwa ya kuanza kufanya maandalizi ili ziweze kuleta ushindani wa kweli ndani ya ligi.


Kila kitu kinawezekana ikiwa kutakuwa na mpango makini na ukweli ni kwamba kupanda ni rahisi na kushuka ni rahisi pia lakini ukishashuka kurudi huku juu huwa inakuwa ngumu.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA CHAMPIONI JUMATATU


Zile ambazo zimeshuka daraja zimekuwa zikipambana kwa muda mrefu kuweza kurudi ndani ya Ligi Kuu Bara. Hii inatokana na utofauti na kuwa kwenye changamoto tofauti katika Ligi Daraja la Kwanza.


 Matukio haya yawe darasa kwa timu ambazo zinapambana kupanda kwenye ligi nazo zinapaswa zijue kwamba huku juu mambo sio mepesi kama ambavyo wanafikiria.


Imani yangu ni kwamba zile ambazo zimepanda zinatambua kwamba kuna ushindani mkubwa kwenye ligi na wanatambua pia lipo suala la kushuka.


Tunataka kuona timu ikipanda kwenye ligi iwe na uwezo na vigezo vya kuhimili mikikimikiki ya huku kwani hakuna kuzubaa ni mwendo wa kukimbizana.


Kikubwa ni maandalizi hakuna jambo lingine ambalo litawafanya waweze kuwa bora katika mechi ambazo watacheza kwa msimu ujao ndani ya ligi.


Jambo lingine ambalo wachezaji wanapaswa kutambua ni kwamba nidhamu ni suala la lazima kwao ikiwa wanahitaji kufikia mafanikio yao kila wakati.


Itawafanya waweze kuwa bora muda wote ndani ya uwanja na kuyafikia mafanikio yao pamoja na yale ya timu kiujumla kwa kuwa inawezekana kufanya hivyo.


Ninaona kwamba msimu ujao ushindani utakuwa mara dufu zaidi ya sasa kutokana na uwekezaji ambao umefanywa hivyo ni suala la kusubiri na kuona mambo yatakuwaje lakini jambo la muhimu ni kujipanga.


Kuna umuhimu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutazama namna ya kuwalinda wachezaji wetu kiujumla hasa kwa timu ambazo zitashuka daraja pamoja na zile ambazo zinashiriki Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili pamoja na zile za mkoa.


 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here