ZIKIWA zimebaki siku mbili kuwakutanisha watani wa jadi, Simba na Yanga Uwanja wa Mkapa, Julai 3, taarifa kutoka benchi la ufundi la Simba limeweka wazi kwamba litawafunga Yanga kwa kanuni.
Mchezo wa awali ulipangwa kuchezwa Mei 8 uliyeyuka baada ya Yanga kugomea mabadiliko ya muda ghafla kwa kuwa awali ulipangwa kuchezwa saa 11:00 kabla ya Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) Cliford Ndimbo kutoa taarifa kwamba kutakuwa na mabadiliko ya muda mpaka saa 1:00 usiku.
Mtoa taarifa kutoka ndani ya benchi la ufundi la Simba amesema kuwa wataingia uwanjani kwa tahadhari ili waweze kuwafunga wapinzani wao kwa kanuni.
“Hamna namna kwenye ligi jambo la msingi ni pointi tatu, sasa ambacho tutakifanya ni kuwafunga wapinzani wetu Yanga kwa kanuni, wao waliondoka na hatujui kilichowakuta basi tusubiri na tuone itakavyokuwa,” ilieleza taarifa hiyo.
Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes amesema kuwa mchezo huo utakuwa mgumu ila watapambana kupata pointi tatu muhimu.
“Utakuwa mchezo mgumu na kila timu inahitaji ushindi hilo lipo wazi tutaingia kwa hesabu za kusaka ushindi na wapinzani wetu tunawaheshimu,” .
Kwenye msimamo Simba ipo nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 73 baada ya kucheza mechi 29 na Yanga ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 67 baada ya kucheza mechi 31.