ZIMEBAKI saa chache kabla ya watani wa jadi, Simba na Yanga kukutana katika mchezo wa Ligi Kuu mzunguko wa pili ukaopigwa kesho Julai 3, kwenye Uwanja wa Mkapa.
Awali mechi hiyo ilipangwa kuchezwa Mei 8 lakini ilisogezwa mbele baada ya kuwepo na mabadiliko ya ratiba ya muda wa kucheza kutoka saa 10 jioni hadi saa 1:00 usiku, mabadiliko ambayo Yanga waliyapinga kuwa ni kinyume na kanuni za ligi hiyo.
Katika saa zilizobaki kocha wa Simba, Didier Gomes ameandaa ratiba maalumu yenye mchanganyiko ndani yake kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya watani zao.
Alisema kabla ya kuanza mazoezi jana alikutana na wasaidizi wake kujadili mambo kadhaa kuelekea mchezo huo ikiwemo kuangalia video za mechi zilizopita za Yanga wakishirikiana na mtaalamu wa kuwachambua wapinzani, Kelvin Mavunga ambaye naye alieleza vingi.
“Kikubwa ambacho tulikuwa tunaangalia ni mambo ya kiufundi kuona namna gani tutayatumia na kuwazidi wapinzani wetu, siwezi kuviweka wazi kwani ndizo silaha zetu.
“Baada ya kukusanya yote kutoka kwa wapinzani tunahamishia uwanjani wakati wa mazoezi ambapo tumeanza maandalizi hayo ya kuhakikisha tunashinda mchezo huo na kuwa mabingwa wa ligi kama malengo yetu ya mwanzo wa msimu yalivyo,” alisema.