BAADA ya GSM kukubali kufanya kazi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, sasa mabosi hao wameelekeza nguvu kubwa katika mchezo dhidi ya Simba utakaofanyika kesho Jumamosi, Uwanja wa Mkapa jijini Dar.
Manji alikuwepo katika Mkutano Mkuu wa Yanga wa kupitisha katiba mpya ya mfumo wa mabadiliko uliofanyika Jumapili iliyopita kwenye Ukumbi wa DYCCC, Chang’ombe, Dar.
Katika mkutano huo, Manji alitoa kauli ya kushirikiana na viongozi wa Yanga waliopo sasa ambapo GSM ndiyo wamekuwa mstari wa mbele kusimamia mambo mengi ikiwemo ishu za usajili na bonasi za wachezaji katika mechi mbalimbali.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Yanga, kimeliambia Spoti Xtra kuwa, uongozi wa timu hiyo umeandaa dau kubwa ambalo litahamasisha ushindi katika mchezo huo.
Mtoa taarifa huyo aliongeza kwamba, baada ya GSM kuweka Sh milioni 300, wanachama wa klabu hiyo wameahidi kuongeza Sh milioni 200 akiwemo Manji na kufanya jumla kuwa Sh milioni 500 ambazo ni nusu bilioni.
“Ni kweli kuna kiasi kikubwa kiliahidiwa na wadhamini wa timu ambao ni GSM kutoa hamasa ya ushindi dhidi ya Simba, waliweka Sh milioni 300 ili Simba wafungwe.
“Hiyo ni baada ya kumalizika kwa Mkutano Mkuu ambapo pia wanachama wengine waliahidi kuongeza dau kuhakikisha Simba inafungwa na Yanga.
“Walioahidi kuongeza fedha hiyo miongoni mwao ni Manji ambapo wenyewe kiasi chao ni Sh milioni 200, hivyo ukiziunganisha kwa pamoja inafika Sh milioni 500,” kilisema chanzo hicho.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Yanga, Dominic Albinus, alisema: “Tunatarajia kuwa na kikao na wachezaji kabla ya mchezo, masuala yote ya bonasi yatafahamika,” .