DIDIER Gomes, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa washambuliaji wake watatu ambao wamefunga jumla ya mabao 37 wanajuhudi kila wakipewa nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza jambo ambalo ni furaha kwake
Safu ya ushambuliaji ya Simba inayoundwa na nahodha John Bocco, Chris Mugalu na Meddie Kagere imefunga jumla ya mabao 37 kwenye mechi 31 ambazo Simba imecheza kati ya mabao 71 ambayo yamefungwa.
Ni Kagere aliyetupia mabao 11, Mugalu 12 na Bocco mabao 14 ikiwa ni safu namba moja yenye ukali kwa kutupia ndani ya ligi kwa msimu wa 2020/21.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Gomes alisema kuwa washambuliaji wake wote wanajituma katika kutimiza majukumu yao ambayo anawaelekeza.
“Ukitazama kuanzia Mugalu yeye ni mshambuliaji anayejituma na kutimiza kazi yake, hiyo ni sawa na ilivyo kwa Bocco na Kagere hili kwangu ni furaha na inatufanya tuweze kufikia malengo.
“Licha ya kwamba wanafanya vizuri ila bado kuna tatizo la kumalizia nafasi ambazo wanazitengeneza kwani hili limekuwa likijirudia, ninadhani kwamba tungekuwa na mabao mengi kwa sasa hasa kwa nafasi ambazo tunazitengeneza,” alisema Gomes/
Kwenye msimamo Simba ipo nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 76 inafuatiwa na Yanga yenye pointi 70 na safu yao ya ushambuliaji imefunga mabao 50 kwenye mechi 32.