Home Yanga SC HONGERA KWA YANGA JUU YA NIYONZIMA, UTARATIBU UENDELEE

HONGERA KWA YANGA JUU YA NIYONZIMA, UTARATIBU UENDELEE


 JANA tulishuhudia utaratibu mzuri walioanza nao Yanga kwa kumuandalia mechi maalum ya Ligi Kuu Bara kwa ajili ya kumuaga, kiungo wao Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.

 

Yanga walimuaga kiungo huyo jana katika mchezo huo wa ligi waliocheza dhidi ya Ihefu FC uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

 

Pongezi nyingi ziende kwa viongozi Yanga walioandaa utaratibu huo wa kumuaga Niyonzima aliyeichezea timu hiyo kwa heshima kubwa na kuipa mataji ya ubingwa tangu ajiunge nayo.


Championi Ijumaa, linaamini huo ni mwanzo mzuri kwa viongozi hao katika kuwajengea heshima kubwa wachezaji wao walioichezea timu hiyo kwa muda mrefu kama ilivyokuwa kwa Niyonzima.


Yanga wanatakiwa kuanzia hapo kwa Niyonzima na wachezaji wengine kama akina Deus Kaseke ambao wamedumu hapo kwa muda mrefu.

 

Lakini sikitiko ni kwamba tunaamini utaratibu huo ungeanza zamani ingekuwa bora zaidi, maana kuna wachezaji kama Kelvin Yondani, Shadrack Nsajigwa na wengine waliondoka kawaida tu licha ya kutumika kwa muda mrefu na kwa mafanikio Yanga.

 

Championi Ijumaa, linaamini kuwa Niyonzima atakwenda kuitangaza vema Yanga nyumbani kwao Rwanda.Awali, ilikuwa ikizoeleka kuwa mchezaji akiachana na timu, basi wanaachana vibaya kwa chuki kitu ambacho ni kibaya hakitakiwi.

Hivyo hawatakiwi kurudi nyuma na badala yake kuendeleza hapo walipoanzia kwa Niyonzima na kuendelea na utaratibu huo mzuri wenye malengo mazuri katika ustawi wa timu.


Tukio hilo ambalo Yanga wamelifanya kwa Niyonzima litawafanya wachezaji waitumikie kwa nguvu timu hiyo wakiamini mwisho wao utakuwa mzuri.

SOMA NA HII  WAKILI WA YANGA, AWAPIGA DONGO HILI SIMBA SC, MANGUNGU AHUSISHWA