Home news ISHU YA UCHAGUZI TFF, MAHAKAMA YATOA MAAMUZI

ISHU YA UCHAGUZI TFF, MAHAKAMA YATOA MAAMUZI


 MAHAKAMA Kuu imetupilia mbali ombi la Ally Salehe la kuzuia mchakato wa uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Akisoma uamuzi wa kesi ndogo namba 305, Jaji Edwin Kakolaki amesema haoni sababu za kuzuia mchakato wa uchaguzi huo wa Agosti 7.

 

Amesema kesi ya msingi ya kupinga kanuni za uchaguzi wa TFF, katiba ya Shirikisho hilo na Zanzibar kutotambulika kwenye masuala ya TFF sasa itasikilizwa na kutolewa uamuzi kabla ya uchaguzi mkuu wa TFF utakaofanyika mkoani Tanga.

 

Ally Salehe miongoni mwa wagombea watatu wa urais wa TFF walioenguliwa katika mchujo wa awali kwa kutokidhi takwa la kikanuni la kuwa na wadhamini angalau kuanzia watano alifungua kesi Mahakama Kuu kupinga kanuni za uchaguzi huo, katiba ya TFF na Zanzibar kutotambulika kwenye masuala ya TFF, wakati huo huo alifungua kesi ndogo namba 305 ya kuomba mchakato wa uchaguzi wa TFF usitishwe hadi kesi yao ya msingi namba 98 itakaposikilizwa.

 

Jaji Kakolaki Julai 17 ametoa uamuzi wa kesi ndogo na kuelekeza kwamba haoni sababu ya kusimamisha mchakato wa uchaguzi huo na badala yake kesi ya msingi iliyofunguliwa na Ally Salehe itasikilizwa na kutolewa uamuzi kabla uchaguzi wa TFF haujafanyika.

 

Nje ya mahakama, Wakili Frank Chacha anayemtetea Ally Salehe alisema Julai 30 kesi yao ya msingi itasikilizwa na pande zote mbili zinapaswa kupeleka vielelezo vyao.

 

“Kwenye kesi ndogo, Mahakama imeona hakuna haja ya kusitisha mchakato wa uchaguzi wa TFF lakini itatoa uamuzi wa kesi yetu ya Msingi kabla ya uchaguzi huo kufanyika na Julai 30 itasikilizwa,”

 

Katika uamuzi wa kesi ndogo, TFF imewakilishwa na mawakili wawili huku Ally Salehe akiwakilishwa na mawakili wake wanne.

SOMA NA HII  AHADI YA RAIS SAMIA YAMFANYA MAYELE KUIBUKA NA HAYA MENGINE...AIKUMBUKA CONGO...