Home Yanga SC NABI APEWA RUNGU, KIKOSI CHA YANGA CHAFUMULIWA

NABI APEWA RUNGU, KIKOSI CHA YANGA CHAFUMULIWA


 UONGOZI wa Yanga umepanga kumpa uhuru wa asilimia 100 kocha wake, Nasreddine Nabi kufanya kile ambacho anaona kitakuwa sawa kwenye kuijenga timu bora kwa ajili ya msimu ujao.

 

Nabi amekuwa na wakati mzuri tangu atue kwenye kikosi cha Yanga, kwani kwenye michezo tisa ambayo ameiongoza timu hiyo, ameshinda mechi saba, sare moja na kufungwa mechi moja. Mchezo wake wa mwisho alimfunga mtani wake, Simba kwa bao 1-0.

 

Kutokana na hilo, vigogo wa Yanga wamefurahishwa na mwenendo wa Yanga tangu Nabi atue kwenye timu hiyo hivyo wanaamini kuwa kama watampa uhuru basi atafanya mara tatu ya hiki ambacho amekifanya kwa kipindi hiki kifupi.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, Thabit Kandoro ambaye aliweka wazi kuwa Nabi ndiye atakayeamua mchezaji gani atoke na yupi aingie kwenye timu na wao wamepanga kumpa kila anachohitaji ili kuweza kuyafikia matarajio.


“Kocha kama Nabi inatakiwa umpe uhuru wa kufanya kazi yake, ukisema umbane na kumuingilia utakuwa unakosea. Sisi viongozi tumeliona hilo na tumempa yeye utawala aseme mchezaji gani anamtaka na yupi hamtaki kisha uongozi utakuwa unafuata matakwa yake,” alisema Kandoro.

 

NABI AIFUMUA YANGA


Licha ya Yanga kubakiwa na michezo miwili ya ligi kuu, tayari Nabi ameanza harakati za kukifumua kikosi hicho kabla ya mchezo wa fainali ya Kombe la FA dhidi ya Simba kwa kuwa wamedhamiria kubeba ubingwa huo.


Nabi amechukua uamuzi huo ikiwa ni siku chache tangu atoke kuifunga Simba hali iliyopelekea Yanga wafanyiwe sherehe kubwa na mdhamini wa timu hiyo wikiendi iliyopita ikiwa ni pamoja na kupanga mikakati ya mchezo huo wa fainali ya FA.

 

Yanga na Simba zitaumana kwenye fainali ya FA Julai 25, kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika kule Kigoma.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya benchi la ufundi la Yanga, zinasema kuwa kocha huyo ameanza kwa kubadili mfumo kwa wachezaji wake kutokana na ugumu wa uwanja watakaokwenda kucheza mchezo wa fanali ili iwe rahisi kwao kuweza kupata matokeo kwani wanaamini hautakuwa mchezo rahisi.

SOMA NA HII  BAADA YA KAUNZA LIGI KWA MOTO WA AINA YAKE...MAYELE ATAMBA KUZIDI KUWAKERA KWA KUTETEMA...

 

“Mwalimu kwanza amesisitiza timu ishinde mechi hizi mbili ambazo zimebakia katika ligi ili timu imalize kwenye nafasi ya pili lakini tayari ameanza kusuka mikakati ya mechi ya Kigoma.

 

“Unajua ni kwamba kitendo cha kuwafunga Simba kimewaumiza viongozi na kwa vyovyote watahitaji kuona wanafanya juu chini washinde jambo ambalo mwalimu amelibaini, sasa anachofanya ni kubadili baadhi ya mambo ya kiufundi ili timu kuweza kupata ushindi kule Kigoma kwa sababu analisisitiza katika mazoezi ya kila siku,” alisema mtoa taarifa.