Home Yanga SC TIMU YA UTURUKI KUILIPA YANGA TSh 924 MILIONI KWA AJILI YA YACOUBA

TIMU YA UTURUKI KUILIPA YANGA TSh 924 MILIONI KWA AJILI YA YACOUBA

 


HUKO Jangwani mambo yanazidi kunoga. Kwa sasa Yanga ni kama kuna vurugu flani ya fedha, kwani tangu klabu hiyo ilipotangaza kupitisha rasimu ya katiba mpya ya mabadiliko yao mfumo wa uendeshaji, fedha zinazidi kukimbilia kwao.

Siku chache baada ya kulamba dili la Sh41 bilioni toka Azam Media, vurugu imehamia kwa mshambuliaji wao Yacouba Songne ambaye wakati wowote anaweza kuingizia mamilioni ya rekodi kutoka kwa Waturuki.

Songne, aliyefungia mabao nane katika Ligi Kuu Bara akiwa ndiye kinara wa Yanga, anatakiwa na klabu moja ya Ligi Daraja la Kwanza nchini Uturuki ambao ofa yao imewafanya vigogo wa Yanga kuitana usiku kuijadili.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba Songné amepewa ofa nzito, lakini Yanga nao wameambiwa kama mtakuwa tayari mtapewa Dola 400,000 (takriban Sh924 milioni) katika uhamisho huo.

Yanga kusikia hivyo wakaitana haraka wakitaka kupandisha kidogo dau hilo, wakitaka kumuongezea mkataba ili utumike kupandisha fedha hiyo.

Hata hivyo, gazeti la Mwanaspoti linafahamu kwamba Songné amegomea hatua hiyo ya kuongeza mkataba na sasa atabakiza mwaka mmoja katika mkataba wake wa miaka miwili aliosaini mwanzoni mwa msimu huu.

Hata hivyo, Yanga ni kama waliwahi kupiga hesabu vizuri za kuchukua mamilioni hayo kufuatia klabu hiyo ya Uturuki walikuwa wakimpigia hesabu muda mrefu, ila walihofia kukamilisha usajili huo wakati wa vita ya covid 19 pale mshambuliaji huyo akiwa Ghana katika klabu ya Asante Kotoko.

“Tutaangalia kipi cha kufanya, zimekuwa zikija ofa nyingi, lakini hii naona itajadiliwa sana, tumekubaliana tukutane kwa kuwa hata meneja wake anaulizia sana tumefikia uamuzi gani,” alisema bosi huyo wa Yanga aliyeomba kuhifadhiwa jina lake.

Mshambuliaji huyo aliyeasisti mara nne, ndiye mshambuliaji tegemeo kwa sasa wa Yanga ambayo ipo nafasi ya pili na ikiwa imetinga fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) ikitarajiwa kuvaana na watani wao, Simba Julai 25 mjini Kigoma.

Kama dili hilo litatiki itaiongezea Yanga mamilioni ya fedha baada ya udhamini ilioupata mapema wiki hii kutoka Azam Media, huku ikielezwa kuna nyingine zipo njiani zikisubiri kukamilishwa na kuifanya klabu hiyo kusahau msoto iliokuwa nao kiasi cha kutembeza bakuli.

SOMA NA HII  KASEKE:TUTAIFUNGA KEN GOLD KESHO

HERSI AFUNGUKA

Akizungumzia juu ya dili hilo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hersi Said alisema wamepokea ofa mbalimbali zinazomhitaji mshambuliaji huyo.

“Tuna ofa nyingi zinazomhitaji Yacouba (Songné) ambazo klabu bado inaendelea kuzifuatilia kwa kuzifanyia kazi, hii kwetu ni ishara kwamba hatukuokota wachezaji, tulitulia na kusaka watu sahihi kwa klabu yetu,” alisema Hersi ambaye kampuni yao ya GSM ndio ilisimamia dili la kumleta Songné pale Jangwani msimu huu akitokea Ghana.

“Yacouba utaona ni kwa kiasi gani ameweza kuonyesha thamani yake ndani ya kikosi chetu mpaka timu hizo kumuona na tutaleta wachezaji bora zaidi katika siku zijazo hapa Yanga,” alisisitiza Hersi ambaye tayari ameshakamilisha dili kadhaa za Yanga ikiwamo ya beki Mkongomani, Djuma Shaaban kutoka AS Vita ya DR Congo.