Home Yanga SC YANGA TUMEMUAGA NIYONZIMA, VIP KUHUSU YONDANI?

YANGA TUMEMUAGA NIYONZIMA, VIP KUHUSU YONDANI?


 KLABU ya Yanga imeonyesha heshima kwa kuamua kutoa mkono wa byebye kwa nyota wake, Haruna Hakizimana Niyonzima raia wa Rwanda.

Niyonzima ameagwa kwa heshima wakati Yanga ikiivaa Ihefu FC iliyokuwa inapambana kuhakikisha inashinda mechi yake dhidi ya Yanga ili ibaki Ligi Kuu Bara.

Yanga wameamua kumuaga Niyonzima kutokana na kazi kubwa aliyoifanya akiwa na kikosi cha Yanga ambacho kimemaliza msimu kikiwa katika nafasi ya pili lakini kimetinga fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports.

Kiungo huyo amefanya mengi makubwa akiwa na kikosi cha Yanga, pamoja na kwamba alilazimika kuondoka mara moja na kurejea tena.

Mara moja, Niyonzima aliondoka na kujiunga na watani wa Yanga, Simba ambako baada ya hapo aliondoka na kwenda zake kwao Rwanda.

Wakati Yanga wakipika kikosi upya walimfuata tena Kigali ambako walizungumza naye na kufanikiwa kumrejesha. Amekuwa na mchango wake wakimaliza nafasi ya pili na fainali ya Kombe la Shirikisho.

Pamoja na yote, Niyonzima ameacha alama wakati wa ile Yanga ya Kampakampa tena ambayo ilikuwa ikitoa mateso kwa watani wake Simba kila mara.

Yanga ambayo ilikuwa ni burudani ya aina yake na kama unakumbuka, wakati anaingia pacha kwenye kiungo alikuwa ni Athuman Iddi Chuji na wakatikisa hasa. Wakati Chuji anaondoka Yanga, Niyonzima aliendelea kutamba na kwa wakati mwingine tena akasumbua akiwa na Thabani Kamusoko, wakiifanya Yanga kuwa gumzo hadi inatinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Bila shaka Yanga wanafanya jambo bora kabisa la kumuaga raia huyo wa Rwanda kutokana na kazi yake nzuri aliyoifanya akiwa na Yanga kwa vipindi hivyo viwili na anakuwa mmoja wa wachezaji wa kigeni waliofanya vizuri zaidi katika Ligi Kuu Bara.

Sasa anaondoka, heshima anastahili na mimi ninauga mkono ingawa nina jambo la kuuliza. Kwamba huu utaratibu mara kadhaa, kuanzia kwa Yanga na baadhi ya klabu zimekuwa zikiona sahihi kuwapa heshima kwa kuwaaga au kuwapongeza wachezaji wanapokuwa wanaondoka na zaidi ni wale wa kigeni.

Kwa Yanga, inaweza kuwa imefanya kwa wazalendo, lakini nawauliza tena, hawaoni wachezaji kama Kelvin Yondani pia walipaswa kuagwa kutokana na mchango wao.

Mfano, wakati akiondoka Niyonzima, ninaamini Yondani angekuwa tayari ameishaagwa. Wakati fulani alikaa nje bila ya timu na Yanga ilimaliza msimu ambapo ingeweza kufanya jambo kwake na kumuaga kwa kuwa alikuwa anastahili kuagwa ili kuonyesha wanajali muda wote wa mafanikio akiwa Yanga.

SOMA NA HII  NYOTA WAWILI YANGA WAIBUKIA DR CONGO

Wakati Niyonzima akitamba akiwa na Chuji, Kamusoko na wengine. Yondani ndiye alikuwa akishikilia jahazi la ulinzi la kikosi cha Yanga. Tena alifanya kazi bora akiwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’,lakini hata baada ya kustaafu kwake,

Yondani aliendelea kupambana akiwa na wachezaji kadha wa kadha mfano wa Vicent Andrew ‘Dante’, Shaibu Ninja, Said Makapu na wengine, akaendelea kuwa tegemeo na mhimili wa ulinzi wa klabu ya Yanga.

Hata wakati ule Niyonzima alipoondoka kwenda kwao Rwanda, Yondani alikuwa bado anaitumikia Yanga. Niyonzima aliporejea na kujiunga na Simba, Yondani bado alikuwa akipambana kukitumikia kikosi cha Yanga. Leo kwenye kuagwa, hakuwahi kupewa hiyo heshima.

Vizuri kufanya kama hicho kilichofanyika kwa Niyonzima lakini vizuri zaidi kuwakubuka waliofanya vizuri na kujituma kwa moyo wao wote kuhakikisha Yanga inapata inachotaka. Tumeona hata Yanga mpya ambayo ilibadili zaidi ya wachezaji 15, bado haijafikia mafanikio ya waliyokuwa nayo katika Yanga ya kina Yondani.

Kama ambavyo nimekuwa nikisema siku zote, timu inapaswa kuendelea kujengwa na msimu ujao unaweza kuwa bora zaidi kwa Yanga kama watajipanga lakini naendelea kuwakumbusha, Yondani ni gwiji nchini, ni mmoja wa wachezaji bora wazalendo kuwahi kutokea nchini na anapaswa kupewa heshima yake.

Inawezekana isiwe kwa Yondani pekee au Yanga pekee, nizikumbushe klabu nyingine, kuwaaga wachezaji wao kwa heshima na hasa wale waliojituma hasa kutaka klabu iwe bora na kushinda, wanapaswa kupewa heshima zao na

tusiwadharau kwa uzalendo wao na mara nyingi nimeona, wako viongozi wengi katika klabu zetu wana hisia za kuwadharau wachezaji wazalendo kwa kuwa tu, wanaona kuwafanya waonekane wakubwa ni kama wao viongozi kujishusha.

Tena wakati mwingine, unakuta kiongozi ana miaka miwili tu ndani ya klabu lakini mchezaji ameitumikia klabu kwa zaidi ya miaka sita hadi nane. Huu si uungwana na haifai kuendelea, badilikeni.