Home Uncategorized TAIFA STARS AFCON, TUNAKICHEKA TUSICHOKIJUA LICHA YA KUWA CHA KWETU

TAIFA STARS AFCON, TUNAKICHEKA TUSICHOKIJUA LICHA YA KUWA CHA KWETU


Na Saleh Ally, Cairo
NILIPITA karibu na vyumba vya wachezaji wa Taifa Stars na kuwaona wengi wao wakiwa wamejiinamia na baadhi yao wakibubujikwa na machozi.


Hili lilinishangaza kidogo, nafikiri kwa kuwa sikuwa nimetegemea kwamba baada ya wao kupoteza mechi dhidi ya Kenya wangejisikia vibaya hadi kububujikwa na machozi.


Wachezaji wanalia lakini kuna mashabiki wanafurahia timu yao kupoteza mitandaoni, jambo linaloonyesha cheko zetu zinatokea wakati tukiwa tumefumba macho kwa kuwa tukiyafungua tutagundua hatua tunayopiga maana tutapata nafasi ya kujiuliza kwa nini au tumefikaje hapa.


Pia tutapata nafasi ya kujiuliza, nyenzo tuliyoipeleka vitani ilikuwa sahihi kwa vita hivi, au tuliona tunaweza kujaribu?
Nikajikumbusha siku mbili zilizopita nilipopita kambini kwao wakati wa mkutano wa waandishi, hakika wengi walionekana wanajiamini watafanya vema.


Ukiangalia mechi dhidi ya Kenya katika michuano ya Afcon, Taifa Stars ndiyo ilianza kwa kufunga mabao mawili na Kenya wakisawazisha.


Mechi hii ilikuwa nzuri na tamu na kila upande ulionekana kupania kushinda kwa kuwa ilikuwa ni Afcon ya Afrika Mashariki mbali na sehemu yenyewe.


Baada ya kila timu kuwa imepoteza mechi yake ya kwanza, kila moja iliamini dhidi ya jirani ingeshinda na kutengeneza ushindi wake wa kwanza katika Afcon kwa maana ya historia.


Kenya wamefanikiwa kuishinda Tanzania na huenda hii ni sherehe yao kubwa kwa kuwa nafasi wanaona ilikuwa kubwa kuigaragaza Tanzania na kinachofuata ni kujaribu tu.


Kenya wanakwenda kujaribu mechi dhidi ya Senegal kama ilivyo kwa Tanzania, watakwenda kujaribu tu hakuna ujanja dhidi ya Algeria na huu ndio uhalisia wa soka la Afrika Mashariki unapokutana na timu za Afrika Kaskazini au Magharibi. Kuna jambo la kujifunza hapa.


Hakuna ambaye anajisifia mafanikio ya jambo fulani leo bila ya kuwa alipitia hatua kwa hatua.


Tanzania na Kenya hazikuwahi kukutana Afcon, ni kwa sababu timu za ukanda wetu zimekuwa hazina nafasi hiyo. Lakini safari hii hadi Burundi ilipata nafasi hiyo, ndiyo maana tumepata nafasi ya gumzo hili na ndiyo hatua nyingine ya maendeleo.


Kwanza tayari kila timu inaamini inapaswa kwenda tena Afcon na kujiamini kumeongezeka kwa kuwa Uganda wameonyesha inawezekana zaidi, Kenya wameanza kupaa lakini Tanzania lazima ifanyike kazi ya ziada.


Lazima tukubali, kilichowafanya Kenya warudi mara mbili na kusawazisha kwa kuwa wana timu bora zaidi yetu na sababu tunazijua.


Timu zinazofanya vizuri ni zile zenye wachezaji wengi wanaocheza nje ya nchi zao. Wanacheza katika ligi bora na uwezo wao ni mkubwa kwa kuwa wanafundishwa mengi bora kuliko wanapokuwa katika ligi za nyumbani hasa ukanda wetu.


Katika kundi la timu nne, Tanzania ndio timu ambayo ilionekana yenye nafasi ya mwisho. Ubora wa Kenya ulionekana kwa kuwa wachezaji wao walionekana kuwa tofauti kiuchezaji ukifananisha na sisi.


Angalia mashambulizi yao lakini hata mbinu za ulinzi. Upande wa Stars pamoja na jitihada za juu sana mfano kipa Aishi Manula, mabeki wa kati kama Kelvin Yondani, lakini bado makosa ambayo yanaonekana yanatokana na uwezo yalikuwepo.


Uwezo wao ni bora na hasa katika kiwango chetu lakini si kiwango hiki cha Afcon na unaweza vipi kuwafanya wawazidi Kenya ambao wameendelea kuwekeza kwa nguvu wachezaji wao kuhakikisha wanatoka na kucheza nje ya kwao!


Achana na nahodha Victor Wanyama ambaye anacheza Tottenham iliyo katika Ligi Kuu England, lakini katika kikosi cha juzi, kati ya wachezaji 11 walioanza ni mmoja tu Francis Kahata ambaye anacheza ligi ya kwao Kenya katika kikosi cha mabingwa Gor Mahia. Waliobaki wote wanacheza nje ya Kenya.


Ukiangalia katika hao 10 wanaocheza nje ya Kenya, ni watatu tu wanaocheza Afrika ambao ni kipa Matasi Patrick kutoka St George ya Ethiopia, Mohammed Musa wa Nkana ya Zambia na David Odhiambo wa Zesco ya Zambia, waliobaki wote wanakipiga barani Ulaya.


Katika kikosi cha Tanzania, wachezaji 11, kulikuwa na wachezaji watano wanaocheza nje ya nchi na kati ya hao wawili ambao ni Mbwana Samatta na Farid Mussa wanacheza barani Ulaya lakini watatu ni Thomas Ulimwengu (JS Saoura-Algeria), Hassan Kessy (Nkana-Zambia) na Simon Msuva anayetokea Difaa Al Jadid ya Morocco.


Hapa kama utatulia unaweza kujifunza tofauti ya Kenya na Tanzania.


Wachezaji waliokuwa benchi upande wa Kenya bado walionekana kuwa bora zaidi kuliko benchi letu hata kama kocha wao alionekana kufanya mabadiliko mengi yaliyokuwa sahihi kuliko wetu.


Hata kama utaona kuna wachezaji wengi wanaotokea katika nchi za Ulaya wakiwa benchi ukiachana na Addi Yussuf upande wa Tanzania ambaye inawezekana bado kocha hajamuamini, lakini Wakenya wanaonekana kuwa vizuri zaidi.


Unaweza kuuliza, vipi mbona Tanzania iliweza kufunga mabao mawili hayo kupitia wachezaji wetu walio nje? Jibu huo ni mfano wa ubora ninaouzungumzia na huenda ulinzi bora zaidi ungeweza kusaidia kuzuia makosa. Achana na hivyo, bado wachezaji wengi wanaocheza nje wangeweza kufanya vizuri zaidi kuwaongezea nguvu walio ndani kwa maana ya msaada mkubwa.Nje wapi? Inategemea lakini tukubali katika nchi za Ulaya ambako ligi zimepiga hatua zinawabadilisha wachezaji kwa maana ya ubora wa uchezaji lakini na muono wa utekelezaji wa kile wanachokitaka.


Simaanishi wachezaji wetu ni wabaya lakini ninasisitiza, kiwango chao kiliishia pale na hiki ndicho tunapaswa kukikubali kwamba kuna upungufu wa kocha katika mambo kadhaa lakini kuna yale ambayo yangeweza kuwa msaada kupitia kwa wachezaji wenyewe.


Wanalia kwa kuwa walikuwa na nia njema na walitaka kushinda mechi hiyo kwa juhudi kubwa sana, hilo halina ubishi lakini kudura hazizidi uwezo ndio maana Kenya walikuwa wanarudisha na walipofanikiwa kutanguliwa ikawa vigumu tena kuwafunga.


Kabla ya mechi ya Kenya na Tanzania, zilicheza Senegal na Algeria ambao walishinda 1-0. Utauona ubora wa mechi ulivyokuwa na ubora wa wachezaji wao.


Kama sisi leo tunaona kuwa na wachezaji Algeria ni jambo kubwa, wao timu nzima ilikuwa na mchezaji mmoja tu kutoka kwao huyu ni Hicham Bouadoui, wengi wote wanatokea nje ya Algeria na barani Ulaya na baadhi barani Asia.Kwa Senegal kikosi chote cha kwanza ni nje ya kwao hali kadhalika wote waliokuwa benchi wanachezea timu za nje ya kwao na hasa barani Ulaya.


Katika kikosi cha kwanza cha Senegal wachezaji wawili wanatokea England, watatu Ufaransa, wawili Italia kama ilivyo kwa Hispania na mmojammoja kutoka Uturuki na Ubelgiji.


Kikosi cha Algeria, wachezaji  11 walioanza, Wawili Ufaransa kama ilivyo England, wawili Saudi Arabia na mmojammoja kutoka Qatar, Tunisia, Uturuki na Italia.


Ubora wa wachezaji unatokana na ubora wa ligi wanazocheza na hili tulikubali. Angalia Senegal, katika michuano ya Afrika hakuna timu yao tishio wala kuisikia inacheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Lakini wao ndio namba moja kwa ubora Afrika kwa kuwa wana wachezaji wengi barani Ulaya na hasa Ufaransa na Ubelgiji.


Angalia Algeria, wachezaji wao bora wengi wanatokea Ulaya, Asia na huenda kwa kuwa wanasaidiwa na lile jambo la uraia mara mbili.


Lazima tukubali, uwezo wetu ulikuwa ni kufika Afcon na kujifunza kama ambavyo imetokea hivi sasa. Juhudi zimefanyika lakini mwisho wake umekuwa hapo.


Kinachotakiwa sasa ni kupambana kuimalizia mechi dhidi ya Algeria kwa muonekano mzuri na baada ya hapo ni kujipanga kufuzu lakini lazima tukubali kurudi nyuma kwamba kwa wachezaji tulionao sasa, hata tukifuzu tena bado tutalaumiana.


Kinachotakiwa sasa ni kuachia vijana waendelee kwenda nje kucheza na kujifunza ubora zaidi kwa maana ya weledi, kwa kuwa wenzetu wamepiga hatua sana.


Tunapowasifia Senegal au Algeria au kwingineko unkweli ulio wazi, tegemeo lao ni hao wachezaji wanaotokea nje. Sisi tunawezaje kufaulu kwa wachezaji wa ndani pekee?


Misri ilikuwa ni timu pekee iliyokuwa ikifanya vizuri na wachezaji wanaotokea kwao hapa Misri. Sasa mambo yamebadilika baada ya kizazi cha kina Abou Trikka, hata wao sasa wanawategemea wachezaji wengi wanaotokea nje licha ya kuwa na moja ya ligi bora barani Afrika.


Tukubali, tuendelee kupeleka vijana wakacheze katika sehemu zilizopiga hatua kisoka ili kuleta mabadiliko katika mpira wetu wa Tanzania, la sivyo tutaendelea kulaumiana, kuweka siasa na mwisho kujicheka sisi wenyewe jambo ambalo ni ujinga wa hali ya juu.Kikosi cha Senegal vs Algeria
Edouard Mendy (Stade De Reims)
Kalidou Koulibaly (Napoli)
Cheikhou Kouyate (Crystal Palace)
Mbaye Niang (Stade Rennais)
Sadio Mane (Liverpool)
Keita Balde (Inter Milan)
Youssouf Sabaly (Bourdeux)
Alfred Ndiaye (Malaga)
Krepin Diatta (Club Bruges)
Papa Ndiaye (Galatasaray)
Moussa Wague (Barcelona)

Kikosi cha Algeria vs Senegal
Adi-Rais Cobos Mbolhi (Ettifaq)
Aissa Mandi (Real Betis)
Djamel Eddine Benlamri (Al Shabab)
Riyad Mahrez (Manchester City)
Mohammed Youcef Belaili (Esperance)
Baghdad Bounedjah (Al Sadd)
Sofiane Feghouli (Galatasaray)
Adlane Guedioura (Nottingham Forest)
Youcef Atal (Nice)
Amir Rami (Stade Rennais) 
Ismael Bennacer (Empoli)


Kikosi cha Tanzania vs Kenya
Aishi Manula (Simba)
Gadiel Michael (Yanga)
Erasto Nyoni (Simba)
Kelvin Yondani (Yanga)
David Mwantika (Azam)
Mbwana Samatta (Genk)
Thomas Ulimwengu (JS Saoura)
Simon Msuva (Diffa El Jadida)
Farid Mussa (Tenerife)
Hassan Kessy (Nkana FC)
Mudathir Yahya (Azam)


Kikosi cha Kenya vs Tanzania
Matasi Patrick (St. George)
Joseph Okumu (Real Monarchs)
Abud Omar (Sepsi OSK)
Mohamed Musa (Nkana FC)
Masika Ayub (Beijing Renhe)
Johana Omolo (Cercle Bruges)
Francis Kahata (Gor Mahia)
Victor Wanyama (Tottenham)
Erick Otieno (Vasalund)
Michael Olunga (Kashiwa Reyson)
David Owino (Zesco United)

SOMA NA HII  BRUNO TARIMO AJIPA UBALOZI NCHINI SERBIA