LICHA ya wawakilishi wa Tanzania, Yanga kuanza kwa sare kwenye mchezo wa kwanza wa Kombe la Kagame waliweza kupambana katika dakika zote 90 kusaka ushindi.
Kiungo mpya wa Yanga, Jimy Ukonge ambaye ametoka ndani ya UD Songo jana alianza kutengeneza pacha yake na nyota wenzake wapya ikiwa ni pamoja na Dickson Ambundo walioanza katika mchezo wa Kombe la Kagame dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi.
Licha ya ubao wa Uwanja wa Mkapa kusoma Yanga 1-1 Nyasa, nyota hao wapya waliweza kuonyesha makeke yao katika kuipambania jezi ya Yanga chini ya Razack Siwa ambaye ni kocha wa makipa ila jana alikuwa na kibarua cha kuwasimamia vijana hao baada ya Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi kuwa mapumziko.
Ni bao la Wazir Junior dk ya 8 kwa kichwa akiwa ndani ya 18 akitumia pasi ya Ambundo aliyetoa akiwa nje ya 18 ikatua kwenye kichwa cha Wazir Junior na bao la Big Bullets lilipachikwa na Chiukepo Msowoya dk 30 kwa penalti iliyosababishwa na Abdala Shaibu, ‘Ninja’.
Katika mchezo huo gumzo kubwa walikuwa ni nyota hao wapya ambao walikuwa wakianza kwa mara ya kwanza na Ambundo alionekana akiwapa tabu wapinzani kwa kuwapiga chenga za maudhi na pasi ndefu za uhakika.
Bado Ambundo ana safari ndefu ya kufanya kwa kuwa mchezo mmoja hauwezi kutoa picha kamili ya kile ambacho anacho ila akishikilia pale alipoanzia atakuja kuwa tegemeo ndani ya Yanga na timu ya taifa ya Tanzania.
Ukonge kwa upande wake naye alianza kuonyesha makeke hivyo kwa kuwa yupo kwenye uangalizi ni muhimu kuona kwamba kama anaweza kuwa fiti jumla hasa kwa kuwa aliwasili siku hiyo ya mechi.
Rekodi zinaonyesha kwamba kipindi cha kwanza alipiga mashuti matatu ambayo hayakulenga lango na alitoa pasi mbili ambazo hazikutumiwa vizuri na washambuliaji wa Yanga ikiwa ni pamoja na Juma Mahadhi.
Pia alipiga kona tatu kwa guu lake la kushoto ambazo zilitaka kuleta bao kwa Yanga ile ya kwanza iliokolewa na kipa Rabson Chiyedwa ya pili Junior alipiga nje ya lango.
Mbali na kiungo huyo mzawa Dickson Job, Kabwili ambaye alionyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea faulo mchezaji wa Nyasa bado aliweza kuonyesha kiwango bora na Ninja walionyesha kiwango bora katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.
Katika mchezo wa jana pia nyota mpya wa Yanga Fiston Mayele alikuwepo Uwanja wa Mkapa kushuhudia wachezaji wa timu yake mpya wakipambana.