SIKU chache baada ya kushusha winga teleza, Peter Banda kutoka Malawi, mabosi wa Simba hawajamaliza kazi kwani, wanajiandaa kumshusha kiungo fundi wa mpira anayekaba na kushambulia, Saido Kanoute kutoka Mali ili kuja kuwa pacha wa Mganda, Taddeo Lwanga.
Kiungo aliyeng’ara kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji waliopo ardhi ya Afrika (CHAN 2020), ni pendekezo la Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes aliyewaagiza mabosi hao kumtafutia kiungo mwenye sifa ya kukaba na kushambulia (box to box), ile aje kucheza pamoja na Lwanga.
SOMA PIA: UKIACHA BANDA..HAWA HAPA NYOTA WENGINE AMBAO GOMES KAAGIZA WASAJILIE CHAP
Awali Gomes aliwaambia mabosi wake hao kuna viungo watatu wenye sifa hizo anazohitaji na wote ni raia wa Mali na ndipo wakaanza kuwafuatilia na kuridhika kabla ya kukubaliana wamchukue Kanoute anayeichezea Al-Ahli Benghazi ya Libya.
Taarifa hiyo kutoka ndani ya Simba inaelezwa rasmi viongozi wao hawakuridhika na viungo wengine wawili ambao majina yao yamekuwa siri na kuvutiwa na uwezo wa Kanoute (24) ili aje kuliamsha na nyota wengine wa mabingwa hao wa Ligi Kuu na Kombe la ASFC.
Hata hivyo, Simba italazimika kubomoa benki ili kumpa Kanoute kwa vile mkataba wake ndio kwanza mpya kwani alisajiliwa Mei mwaka huu na utadumu hadi mwaka 2024, japo bilionea wa klabu hiyo, Mohamed ‘Mo’ Dewji alikaririwa hivi karibuni kuwa wakimtaka mchezaji yeyote lazima wambebe ili kutimiza malengo.
Simba iliyofika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa misimu miwili ndani ya miaka mitatu, imepania kutwaa ubingwa wa Afrika, hivyo imekuwa ikisaka wachezaji wenye uwezo wa kutimiza hilo na hasa ikizingatiwa inatarajia kuvuta mkwanja wa maana kwa kumuuza Luis Miquissone kwa Al Ahly ya Misri.
“Kuna mazungumzo yameanza kufanyika kati yetu Simba na Al-Ahli Benghazi ili kuona namna gani tunaweza kumpata Kanoute aliyetumikia mkataba wake kwa msimu mmoja tu katika kikosi hicho,” alisema Mjumbe mmoja wa Bodi ya Simba, bila kutaka kutajwa jina gazetini na kuongeza;
“Ndio kwanza tumeanza mchakato wa kumpata Kanoute na shida kubwa mchezaji huyo alisaini mkataba wa miaka mitatu kwa timu anayoitumikia na uzuri ni tangu amefika Benghazi ameonekana kutokuwa na furaha na hiyo ni sababu kubwa kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara jambo ambalo kama watakubali kumuachia kwetu tutamtumia zaidi kuliko huko.”
Kanoute alijiunga na Benghazi Mei 3, 2021 kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Stade Malien iliyopo Ligi Kuu ya Mali na mkataba wake utamalizika Desemba 31, 2024.
SOMA PIA: WAKATI LUIS AKIIBUKIA AL AHALY… MUGALU HUYOO APATA SHAVU TIMU KUTOKA MOROCCO
Katika hatua nyingine Simba imeamua kutega mingo zao kwa kiungo wa AS Vita, Amede Masasi ili kama itatokea watamkosa Kanoute wamchukue Mkongoman huyo kuja kumsaidia Lwanga.
“Kama ikitokea tumeshindwa kumpata Kanoute maana yake tutamueleza (Gomes) na kurudi kwa Masasi aliyemkataa awali au kumtafutie mwingine anayeweza kukithi mahitaji ya timu kwa kocha huyo,” alisema kigogo huyo na kuongeza;
“Hata hivyo, tunapambana mno kumchukua Kanoute, kwani ndiye chaguo sahihi, ila ikishindikana kuna njia ya pili ya kumsainisha mbadala wake, ili kuimarisha kikosi.”