WAKATI kukiwa na tetesi za kutakiwa BS Berkane ya Morocco inayonolewa na Kocha Florent Ibenge, straika wa Simba, Chris Mugalu aliyemaliza msimu uliopita na ambao 15 nyuma ya nahodha wake, John Bocco amesema amepata akili mpya anayopanga kuitumia msimu ujao ili atupie zaidi katika Ligi Kuu Bara.
Mugalu alisema katika msimu uliopita hakuwahi kukutana na mabeki wepesi, licha ya kupambana kiume na kufunga idadi hiyo ya mabao kupitia michezo michache, lakini akisema kuwa, ugumu huo umemfanya sasa ajipange ili arejee kivingine msimu ujao akiwa bora zaidi.
“Siwezi kumtaja beki mmoja kwamba ndiye alikuwa bora zaidi, walinikaba kama inavyotakiwa nami nikatumia ujanja na kufanikiwa kufunga mabao 15 na niseme wazi ilihitaji maarifa mapya kila nilipopewa nafasi na kwa msimu ujao nitakuwa mahiri zaidi ili nisikwamishwe kwenye ndoto za kubeba tuzo,” alisema.
“Natamani ndoto ya kuchukua kiatu ambayo sikuifanikisha msimu uliopisha niitimize msimu ujao licha ya kwamba ushindani utakuwa mkubwa. Hongera kwa nahodha wangu Bocco aliyeibuka mfungaji bora,” alisema Mugalu aliyesajiliwa na Simba msimu uliopita akitokea Zambia.
Aliongeza kila alipokuwa anapewa nafasi ya kucheza alijiwekea malengo ya kumuaminisha kocha wake Didier Gomes kwamba hajakosea kumpanga, jambo lililokuwa linampa hamasa zaidi.