Straika Kadina Kabangu wa Motema Pembe na timu ya Taifa ya DR Congo amezungumza na viongozi wa Simba na huenda wakamshusha jijini Dar es Salaam ndani ya siku mbili zijazo.
Simba ambao jana waliondoka kundi la kwanza kwenda kambini Morocco wanamchukua mchezaji huyo kama mbadala wa Meddie Kagere ambaye safari imemkuta.
Habari zinasema kwamba Simba ambao kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa wamekuwa wakihusishwa na mchezaji huyo mwenye mwili mkubwa, wamefanya mazungumzo naye mara kadhaa wiki hii na juzi jioni wakamalizana wakamwambia akae mkao wa safari ya kuja kusaini.
Simba wanaamini fiziki na uwezo wa kufunga wa mchezaji huyo utawabeba kwenye michuano ya kimataifa inayoanza Septemba 11 mwaka huu.
Habari za ndani zinasema kwamba Kabangu safari hii amelainisha masharti na amekubali kwa wepesi kutua Dar es Salaam baada ya kuona mastaa wengi wa DR Congo wanakimbilia Tanzania na wanatoka kimaisha baada ya muda mfupi.
Habari zinasema kwamba Simba pia huenda ikamuuza straika wake, Chris Mugalu muda wowote kama dili lao na Berkane litakubalika.
Pamoja na mastaa wengine, Berkane chini ya kocha wao Florent Ibenge wanaamini wakimpata Tuisila na Mugalu pamoja na mashine nyingine za Kiarabu Afrika itasimama msimu ujao katika vita ya kuwania kuutingisha utawala wa mabingwa mara 10 wa Afrika, Al Ahly.