KAIMU Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ezekiel Kamwaga ameweka wazi kuwa ataondoka katika nafasi hiyo mara tu baada ya muda aliopewa wa miezi miwili kukaimu kukamilikia.
Kamwaga ameeleza hayo alipofanya mahojiano na mtangazai Oscar Oscar wa EFM ,ambapo alisema anamambo yake binafsi ya kufuatilia nchini Uingereza.
Julai 28, mwaka huu Bodi ya Wakurugenzi ya Simba ilimtangaza rasmi Ezekiel Kamwaga kushika nyadhifa ya Kaimu wa Idara ya habari na mawasiliano wa klabu hiyo, kuifuatia kuondoka kwa aliyekuwa Msemaji wa Simba, Haji Manara.
Akizungumzia majukumu yake ndani ya Simba, Kamwaga amesema: “Watu wengi wanauliza kwanini nimekaimu nafasi hii kwa miezi miwili pekee, licha ya kwamba nina uzoefu wa kutosha wa kusalia kwa muda mrefu zaidi, na labda ikiwa nitaendelea na majukumu haya baada ya muda niliopewa kukamilika.
“Lakini ningependa kuweka wazi makubaliano yangu na Uongozi wa juu wa Simba ni kushikilia nafasi hii kwa miezi miwili, na siwezi kuongeza hata siku moja mara baada ya muda huo kukamilika.
“Hii ni kwa sababu nina majukumu yangu binafsi ambayo natakiwa kuyafanya nje ya Tanzania, lakini kabla ya kuondoka ni lazima nihakikishe nimekamilisha kazi ya kufanikisha mchakato wa kumtafuta msemaji mpya.”