YANGA tayari beki wao mpya Yannick Bangala yuko kambini lakini kocha wao mmoja wa zamani akaibuka na kusema kisiki hicho hakina tofauti kubwa na mkongwe wao wa zamani Kelvin Yondani.
Akizungumza kutoka Ufaransa, Kocha Mwinyi Zahera alisema hatua ya Yanga kumpata Bangala ni ingizo bora katika timu yao na kwamba beki huyo amekomaa kiuzoefu na ana ubora mkubwa.
Zahera alisema, Bangala anayemfahamu hana tofauti kubwa sana na Yondani kutokana na mtindo wao wa uchezaji, ila ana uzoefu mkubwa katika kucheza katika mataifa mbalimbali.
Kocha huyo Mkongomani alisema Bangala ndani ya Yanga atakuwa na faida kubwa akiungana na mabeki wenzake ambapo ubora wake mkubwa ni kujua kuwapanga wenzake na kuanzisha mashambulizi.
“Yanga wamempata Bangala ni hatua nzuri sana huyu ni beki bora sana atawasaidia ana uzoefu wa kutosha na amekomaa vizuri atawasaidia zaidi wakienda kwenye mashindano ya kimataifa,” alisema Zahera na kuongeza; “Bangala anajua sana kucheza mipira ya juu anajituma sana. Ninavyomfahamu Bangala naona kama Yanga imempata Kelvin (Yondani) mwingine lakini huyu ni hodari zaidi.”