ALIYEKUWA mlinda mlango wa Yanga, Metacha Mnata anakaribia kumalizana na KMC kwa ajili ya kuwatumikia kwenye msimu ujao wa 2021/22.
Metacha anatarajiwa kujiunga na KMC kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga, ambayo ilitangaza rasmi kuachana na kipa huyo pamoja na Mkenya Faroukh Shikalo Agosti 9, mwaka huu.
Nyota huyo ambaye ni miongoni mwa wachezaji walioitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars, ameichezea Yanga aliyojiunga nayo Agosti 8, 2019 kwa misimu miwili.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Meneja wa Metacha, Jemedari Said alisema: “Mpaka sasa kuna ofa sita za timu ambazo zinahitaji huduma ya Metacha, timu tano ni za hapa nyumbani huku timu moja ikiwa ni ya nje ya nchi.
“Kuhusiana na KMC ni kweli ni miongoni mwa timu ambazo tupo kwenye mazungumzo nazo, siwezi kuweka wazi kuhusu wapi tumefikia katika mazungumzo hayo lakini muda ukifika kila kitu kitakuwa wazi, nikuhakikishie kuwa Metacha hawezi kukosa timu ya kucheza msimu ujao, .”
Ulipotafutwa uongozi wa KMC kuzungumzia mipango yao ya usajili, Ofisa habari wao, Cristina Mwagala alisema: “Kwa sasa siwezi kuzungumzia taarifa za mitandaoni, lakini niwahakikishie kuwa hivi karibuni tutatoa taarifa rasmi ya usajili mzima.”