RAIS Samia Suluhu Hassan, amekubali kuwa mdhamini wa michuano ya Kombe la CECAFA Wanawake, linalozishirikisha timu za nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, zilizo chini ya Baraza la Vyama vya Soka vy ukanda huu.
Akizungumza jana Ikulu, Dar es Salaam kwenye halfa ya kuipongeza timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 23 iliyotwaa Kombe la CECACA kwa umri huo Julai 30, mwaka huu nchini Ethiopia, pamoja na wanariadha walioiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Olimpiki hivi karibuni, Tokyo nchini Japan, Rais Samia alisema amekubali kuwa mdhamini baada ya ombi la Rais wa Shirikishisho la Soka nchini ambaye ni Rais wa sasa wa CECAFA, Wallace Karia kutaka kufanya hivyo, kama ambayo Rais Paul Kagame amekuwa akidhamini michuano ya Kombe la CECAFA kwa Klabu Bingwa za Ukanda huu, na kupachikwa jina la Kombe la Kagame.
“Kuna ombi tulinong’ona na Mheshimiwa Rais wa TFF, wanataka kuanzisha CECAFA ya Wanawake, lakini mashindano haya wanataka udhamini, akanitolea mfano mwenzako Kagame anadhamini michuano fulani huko, sasa itakuwa vema na wewe ukadhamini haya,” alisema Samia na kuongeza.
“Nikamuuliza hebu niambie kiasi gani niangalie misuli yangu, akanitajia hicho kiasi ambacho sitaki kukisema hapa, lakini nimepima misuli yangu, nikaona mwenyewe sitaweza, lakini nitajua nitakapozipata.
Kwa hiyo niwatangazie kuwa nitadhamini haya mashindano,” alisema na kusababisha waliohudhuria hafla hiyo kupiga makofi kuonyesha kufurahi kwa kukubali ombi hilo.
Mbali na hilo, Rais aliipongeza timu ya Taifa ya Vijana U-23 kwa kuchukua Kombe la CECAFA, pamoja na wanariadha wa Tanzania walioiwakilisha nchini kwenye michuano ya Olimpiki mwaka huu huko Tokyo nchini Japan.
“Kwa kazi kubwa mlioifanya mwaka huu, ni imani yangu kila mwaka sasa mtakwenda na mwendo huo, nihitimishe kurudia kuhimiza timu zetu za michezo zitakazoshiriki michuano ya kimataifa, pamoja na zile za watu wenye ulemavu na klabu mbalimbali kujiandaa vema na kucheza kwa kujituma ili kupeperusha vema bendera ya taifa letu.”