MAHAKAMA ya usuluhisho masuala ya mpira kimataifa ‘CAS’ imesogeza mbele hukumu ya kesi kati ya Klabu ya Yanga dhidi ya mchezaji Benard Morrison iliyokuwa isikilizwe Agosti 24,2021 huku wakiomba samahani kwa kushindwa kusikiliza shauri hilo.
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na CAS ikisainiwa na mshauri wao, Caroline Fischer imeomba radhi kwa pande zote mbili na kusogeza kesi hiyo mpaka Septemba 21,2021.
“Kwa niaba ya Rais wa mahakama ya usuluhisho (CAS) tunaomba pande zote mbili zipokee samahani ya kuchelewa kwa kutolewa rasmi maamuzi ya kesi, bado inafanyiwa kazi kwa kutoangalia upande wowote,”imesomeka taarifa hiyo iliyoandikwa na Fischer.
Morrison ishu yake ni kuhusu usajili ambapo Yanga walifungua kesi kwa kile walichoeleza kuwa mchezaji huyo alisaini ndani ya Simba akiwa na mkataba.
Mchezaji mwenyewe anadai kwamba alisaini dili akiwa mchezaji huru kwa kuwa alikuwa amesaini dili la miezi sita ambalo lilikuwa limemeguka.