Home Azam FC ILE ISHU YA AZAM FC KUBADILI LOGO …KUMBE NYUMA YA PAZIA SABABU...

ILE ISHU YA AZAM FC KUBADILI LOGO …KUMBE NYUMA YA PAZIA SABABU NI HIZI HAPA


KLABU ya Azam FC imezindua nembo mpya ya timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2021-22 na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ alisema kuwa lengo kuu la kuzindua nembo hiyo ni kutaka kuitangaza timu hiyo kisasa wakati huu wakielekea kwenye michuano ya kimataifa huku akiweka wazi kuwa malengo yao makubwa kama klabu ni kufika kwenye hatua ya makundi katika Kombe la Shirikisho Afrika (CC).

“Maandalizi hayaanzii tu kwa wachezaji ni mfumo ambao unaanzia kwenye kila idara na ndio maana tumeamua kuzindua logo yetu mpya ambayo itaitangaza timu yetu kwenye michuano ya kimatifa lakini pia sisi kama viongozi tumejiwekea malengo ya kuhakikisha tunafika mbali zaidi ingawa hatua ya makundi ndio kipaumbele chetu cha kwanza,” alisema.

Mgeni rasmi katika tukio hilo alikuwa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, ambaye ameipongeza timu hiyo kwa hatua iliyofikia tangu ilipoanza rasmi kujulikana na kuwaahidi kushirikiana na uongozi katika kutengeneza ajira nchini.

“Uwekezaji kwenye Azam FC umetoa fursa kubwa sana ya ajira kwa vijana, wachezaji na madaktari na kama Azam walivyosema wametoa ajira ya zaidi ya watu 120 hivyo ni jambo la kupongezwa na sisi kama Serikali tunaahidi kutoa ushirikiano ili kuongeza fursa zaidi za ajira kwa vijana nchini,” alisema.

Katika hatua nyingine Bashungwa alisema kuwa anaipongeza Azam media kwa uwekezaji wake katika soka la Tanzania kwani limeongeza nguvu kwa klabu kwa miaka 10 ijayo huku pia akiipongeza Shirika la habari Tanzania (TBC) kwa kuingia mkataba na TFF kwenye thamani ya Sh3 bilioni, kwa miaka 10 kwa ajili ya utangazaji wa mechi kwa njia ya sauti.

“Mabiliano yaliyowekwa na Azam media na TBC yataleta tija kwa klabu zetu kwenye uendeshaji tofauti na miaka ya nyuma ambapo klabu zilikuwa ombaomba,” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Rais wa TFF katibu mkuu wa (TFF) Wilfred Kidau alisema kuwa anaipongeza Azam FC kutokana na mchango wao mkubwa kwenye soka la Tanzania na kuahidi kuendelea kushirikiana kwenye fursa mbalimbali kwa mafunaa ya Mpira wa Miguu.

SOMA NA HII  AZAM FC WAANZA KULIFUKUZIA JAMBO LAO

“Azam wamekuwa wadau wetu kwenye maendeleo ya soka nchini na hivyo sisi kama shirikisho tutaendelea kushirikiana ili kuona Mpira wetu unafikia mbali zaidi,” alisema.

Katika uzinduzi huo wageni mbalimbali walihudhuria wakiwemo Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia na Katibu wake Mkuu Wilfred Kidau.

Wengine waliohudhuria ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha na Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamisi Taletale maarufu kama Babu Tale.