Home Yanga SC ISHU YA USAJILI YANGA YAPEWA ONYO

ISHU YA USAJILI YANGA YAPEWA ONYO


 TAYARI Yanga wameamua kuanza usajili kwa ajili ya msimu mpya wa 2021/22 ambao utakuwa na matarajio makubwa kwa Wanayanga.

 

Nasema Wanayanga kwa kuwa Klabu ya Yanga inaendeshwa na nguvu za wanachama na linakuwa ni jambo kubwa sana kuangalia nguvu yao wakati wanapokuwa na uhitaji.

 

Misimu minne sasa Yanga haijawahi kugusa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, jambo ambalo hata kama watakuwa hawalisemi sana lakini wanachama na mashabiki wa Yanga, litakuwa limewachosha.

 

Wanataka na wenyewe kuona timu yao inabeba ubingwa ambao unatambulika kama sehemu ya michuano sahihi inayotambulika.Tunajua, ukiachana na Ngao ya Jamii kuna ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam Sports.


Yanga wamekuwa wakisuasua upande huu huku watani wao Simba wakiendelea kuchanua.Unaona, hata nafasi ya kwenda katika michuano ya kimataifa inaonekana imekuwa kwa “msaada wa Simba”, jambo ambalo kwa sasa wanaweza kuwa wanalichukulia kama mzaha lakini bila ya ubishi, watakuwa wamechoka.

 

Inawezekana kabisa uvumilivu wao sasa umefikia ukingoni na tamaa yao ni kuona Yanga inafanya vizuri na kunaweza kukawa na ugumu sana kwa kuwa matumaini makuu kwa mashabiki na wanachama wa Yanga, wamewekeza katika msimu huu ujao.

 

Msimu ujao ndio wamejaza kila kitu wakiwa na imani kubwa kwamba mambo yataamka, kwamba viongozi wao wanaelewa wanachohitaji na wanajua kabisa kwamba kuna marekebisho yatafanyika kuhakikisha wanafikia mafanikio ambayo wameyasubiri kwa wakati au muda mrefu sana.

 

Kumekuwa na maneno fulani hivi ya kuwapa matumaini, kumekuwa na maneno ambayo yamewafanya waamini kesho kuna jambo bora linakuja.

 

Ninaamini, kama Yanga itashindwa kubeba kikombe chochote kwa msimu huu ujao, hakika suala la kukata tamaa litachukua nafasi kubwa sana.Kiasili, inajulikana kuwa mashabiki wa Yanga si wavumilivu sana lakini kwa safari hii mambo yamekuwa tofauti kidogo.

 

Uvumilivu wa kipindi cha misimu minne hauwezi kuwa wa muda mfupi na lazima tutoe nafasi ya kuwapongeza mashabiki wa Yanga kwa kuwa wamejitahidi sana.

SOMA NA HII  KWA USALAMA WAKO...IKIFIKA DK YA 80 UKICHEZA NA YANGA HII YA GAMONDI AMUA KUPAKI BASI TU..

 

Angalia timu ambayo haijabeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu minne lakini hawajawahi kuacha kwenda uwanjani na wamekuwa wakiendelea kuishangilia timu yao kila kukicha. Uzalendo wao hauna mfano na wanapaswa kupongezwa.

 

Wakati tunawapongeza mashabiki na wanachama wa Yanga, huu ndio wakati mwafaka wa kuwakumbusha viongozi wa Yanga tukianza na wale ambao wanahusika na usajili kwamba, makosa basi na msimu huu ni wa jambo la lazima iwe kombe au makombe.

 

Hakuna mjadala, msimu huu lazima Yanga wafanye jambo kwa kuhakikisha wanabeba kombe au makombe, la sivyo hawatakuwa na jambo au njia yoyote ya kujitetea na kutokea sehemu iliyo huru ya kusema “tumekosea tena”.

 

Simba wamejenga timu yao kwa muda mfupi na inaonekana kwa muda mfupi wamejenga kikosi chao kilichofanya vizuri kwa misimu minne mfululizo.

 

Lakini vipi Yanga kwa siku zote walizokuwa hawachukui mataji, maana yake walikuwa wanajiandaa na hata baada ya kushindwa kubeba ubingwa mara kadhaa walifanya mabadiliko.

 

Msimu mmoja kabla, walipangua karibu kikosi chote na kikosi chao kipya kikaishia nafasi ya pili nyuma ya Simba, mara mbili.

 

Sasa si wakati wa kujenga tena kikosi bila ya mafanikio na lazima hili liwe katika vichwa vya viongozi hao.Lazima tuone mafanikio ili kuonyesha kweli kuna ngazi walikuwa wanakwenda kwenye mabadiliko sahihi ya ubora.


 Hakuna ujanja, Yanga lazima wafanye vizuri hata kwa asilimia 60 kuonyesha kweli wanapiga hatua na usajili wao unapaswa kuwa usajili sahihi.

 

Yanga hawapaswi tena kubahatisha, hawapaswi tena kwenda mwendo usio na mafanikio na kama kujipanga basi kumetosha na huu
ni msimu wa kuonyesha 
wamejifunza kutokana na makosa na huu ni wakati wa kuonyesha ubora wao na kuangukia katika mafanikio.