Home Makala KIZAZI CHA AZAM FC KILICHOCHEZA KAGAME KITUNZWE, WENGINE WAGANDAMIZIE

KIZAZI CHA AZAM FC KILICHOCHEZA KAGAME KITUNZWE, WENGINE WAGANDAMIZIE


 MOJA ya mchezo matata na uliokuwa na ushindani mkubwa kwenye Kombe la Kagame 2021 ni ule wa hatua ya nusu fainali uliochezwa Uwanja wa Azam Complex.

Ilikuwa ni Azam FC ya Tanzania dhidi ya Big Bullets ya Malawi. Ulipigwa mpira wa kitabuni uliokuwa unajibu kupitia miguu ya vijana wa Azam FC.

Licha ya kwamba walikwama kupenya hatua ya fainali walitoa burudani ile ambayo ilikuwa inatakiwa kuonekana siku ya fainali.

Namna vijana walivyokuwa wakicheza kwa kujituma na kupambania jezi ya Azam FC na taifa kiujumla ilikuwa ni burudani. Zile dakika 90 za mwanzo zilipomeguka na ubao kusoma Azam FC 2-2 Big Bullets, hakika ilikuwa burudani tosha.

Dakika 30 za nyongeza pale ilikuwa ni mbinu ya kujilinda zaidi lakini mwisho wa picha ilikuwa ni Azam FC kufungashiwa virago kwenye mashindano ya Kagame katika kusaka nafasi ya kutinga hatua ya fainali.

Penalti wanasema hazina mwenyewe lakini inawezekana maandalizi yakiwa bora katika eneo hili pia Azam FC wanaweza wakawa imara kwani kupoteza kwa kufungwa penalti 4-2 ni maumivu kwa Watanzania.

Yote kwa yote neno langu ni kwamba kile kizazi ambacho kilicheza Kombe la Kagame kitunzwe kwa kupewa nafasi ya kucheza kwa muda mrefu zaidi ili kuwa na ule muunganiko mzuri.

Tunaona kwamba kwa sasa ni Azam FC ambao wamekuwa na mwendelezo mzuri kwenye uwekezaji kwa vijana kama ilivyo kwa Mtibwa Sugar ya pale Morogoro. Katika hili pongezi wanastahili.

Uwekezaji kwa vijana unaleta manufaa kwa taifa kiujumla kwani kwa sasa wengi ambao wanafanya vizuri uwanjani kwa wazawa wamepita kwenye mikono ya watu wa Azam FC ama Mtibwa Sugar.

Kikubwa ambacho kinatakiwa kwa timu nyingine ni kuweza kugandamizia mpango kazi wa timu hizi ili kuwa bora na wasipate tabu inapofika wakati wa kuboresha vikosi vyao.

Simba ni stori yao ya muda mrefu juu ya hazina ya wale vijana ambao walitengenezwa zama za Seleman Matola ambao ni Ibrahim Ajibu, Miraj Athuman, Said Ndemla, Jonas Mkude.

SOMA NA HII  EDO KUMWEMBE:- SIMBA WALIJITOA WENYEWE LIGI YA MABINGWA.....AGUSIA 'HUJUMA ZA MAGORI'

Baada ya hawa hakuna kizazi kingine ambacho kinafanya vizuri huku Yanga wakiwa kwenye mwendelezo mzuri wa vijana lakini  bado hawajaweza kuwa na kituo chenye nguvu kama Azam FC.

Zile pasi za kugonga ambazo Watanzania waliziona kwenye mchezo wa nusu fainali zinapaswa ziishi muda wote ili kuwa na kizazi cha dhahabu hapo baadaye.

Nilipata muda wa kuzungumza na Ofisa Habari wa Azam FC, Thabit Zakaria alibainisha kwamba ni furaha kuwa na vijana ambao wanafanya vizuri licha ya kutukuwepo kwa wale wachezaji wa timu kubwa waliocheza Kagame 2021.

Basi ni wakati wa timu nyingine nazo kugandamizia mpango kazi wa Azam FC pamoja na Mtibwa Sugar ili kuwa na uimara kwenye soka letu Tanzania.

Kuishia nafasi ya nne isiwaumize moyo vijana wana muda wa kufanya vizuri wakati mwingine kwa ajili ya kufanya vizuri zaidi.