Home news RAIS SAMIA AMWAGA NEEMA KWENYE MICHEZO..SIMBU ATAJWA

RAIS SAMIA AMWAGA NEEMA KWENYE MICHEZO..SIMBU ATAJWA


Rais Samia Suluhu Hassan ameanika mipango ya Serikali kwenye michezo huku akieleza kwamba, wataendelea kutunisha mfuko wa maendeleo ya michezo.

“Tumeanza na Sh1.5 bilioni mwaka huu, lakini tutaendelea kutunisha kupitia vyanzo mbalimbali ili uwe na fedha za kukidhi sekta hiyo nchini,” amesema Rais Samia jana katika hafla ya chakula cha mchana na wanasoka wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 23 na wanariadha walioshiriki Olimpiki.

Katika hafla hiyo iliyokwenda sambamba na kupokea kombe la ubingwa wa Afrika Mashariki na kati kwa timu ya vijana, Rais Samia ameeleza dhamira ya Serikali kuwa ni kukuza sekta ya michezo nchini.

“Michezo ni afya, lakini pia ni ajira na inakuza hadhi ya taifa, tunahitaji mafanikio katika sekta hii ndiyo sababu tumeanzisha mfuko wa maendeleo,” amesema.

Amesema pia kwenye kuondoa kodi, wameanza na nyasi bandia lakini watangalia na mengine.

“Tunataka viwanja viwe vizuri, tutakwenda kwenye vifaa na kuangalia kimoja baada ya kingine.

“Tuna mpango wa kujenga akademia ya michezo kwenye chuo chetu cha michezo Mallya, Mwanza, pia kujenga viwanja vitatu vya kisasa vya mazoezi kwenye mikoa ya Geita, Dar es Salaam na Dodoma.

“Pia kujenga sports arena kwani hili ni ombi la muda mrefu la wanamichezo, tunasubiri tupate gharama na tuone wapi tutatoa pesa za ujenzi wa kituo hicho kwani lengo si kujenga kimoja, bali viwili Dar na Dodoma,” amesema.

Ataka maandalizi bora kwa timu za Taifa

Rais Samia ametaka maandalizi bora kwa timu za taifa zinapojiandaa na mashindano ya kimataifa.

Rais Samia amesema wanamichezo wanakuwa na ari na mori kutokana na matendo ya viongozi na kama watavunjwa moyo, miguu yao itapata ukakasi wa ushindani.

“Twiga Stars na Taifa Stars (timu za soka za taifa za wanaume na wanawake) zinajiandaa na mashindano ya Cosafa na ya kufuzu kombe la dunia hivyo wafunzwe vema na wizara iwe tayari kusaidia.

“Vijana wa wavu wanajiandaa na mashindano ya Afrika, lakini pia soka ya walemavu tutakuwa mwenyeji wa mashindano ya Afrika, pia wajiandae vema.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI NA SIMBA..KAZE AVUNJA UKIMYA YANGA....JULIO AKUBALI YAISHE..ADAI YANGA NI BABA LAO...

Katika hafla hiyo ambayo iliwashirikisha viongozi mbalimbali wa wizara ya michez, Baraza la michezo, RT, TOC na TFF, wanariadha wa Olimpiki na timu ya soka ya vijana chini ya miaka 23, rais Samia alitaka kujipanga kuwa na mikakati wa mashindano ya kimataifa.

“Taifa kubwa kama letu kuwakilishwa na wachezaji wachache duniani ni aibu, Tanzania tunaweza kudhalisha wanamichezo wengi.

“Kuna majeshi na kwingine, tufanye kazi nao, mfano jeshini ukiacha Simbu (Alphonce) wapo wengine, tuwaibue walioko huko tuwatengeneze watuwakilishe.

“Kuna mikoa tukatafute vipaji, tuwe na wengi, sio kwenye mashindano wanakwenda wachezaji watatu viongozi 11, tunaenda kushiriki au kutembea? angalau basi wachezaji wangekuwa 6 na viongozi 11, siwalaumu lakini turekebishe.

“TOC ijifanyie tathimini ili kwenye michezo ya Paris ushiriki uwe mkubwa, mwisho wa mashindano ndiyo mwazo, makamu na timu yako mjipange,” amesema.

Ametaka pia utawala bora kwenye vyama na mashirikisho ya michezo nchini kunyooka ili kuwatia moyo na kuiagiza BMT kusimamia hilo.

Avunja ukimya kuhusu masumbwi

Rais Samia amevunja ukimya kuhusu masumbwi na kueleza kwamba japo ni mchezo ambao haupendi, lakini una hamasa.

“Vitasa ni mchezo ambao siupendi, lakini unaleta hamasa kubwa, kina mama nao wanatoka na kutambiana kweli kweli.

“Mimi nikimuona mtu anapigwa ngumi naumia, ndiyo sababu siupendi tu, ila hamasa yake ni kubwa,” amesema rais Samia akiipongeza Azam Media kwa kujikita kwenye michezo hasa soka na ngumi.

Aidha amewasihi wazazi kuwa na moyo wa kuwahimiza watoto washiriki michezoni na kufanya mazoezi.

“Watu wanasema hakuna kungwi mchafu, japo binafsi sipati nusu saa ya kufanya mazoezi kwa siku ila nina afya njema,” amesema rais Samia kwa utani akiwahimiza watu kufanya mazoezi.

Amewataka wadau na wafanyabiashara nchini kuangalia fursa wakati wa mashindano yajayo ya kombe la dunia huko Qatar.

“Hapa na Qatar si mbali, tunafahamu mashindano hayo yataingiza watu wengi, hivyo tujipange kuitumia hii nasi hata kwenye utalii pia,” amesema.