Home Makala TUWAKEMEE WANAOINGILIA MAAMUZI YA BENCHI LA UFUNDI KWENYE USAJILI

TUWAKEMEE WANAOINGILIA MAAMUZI YA BENCHI LA UFUNDI KWENYE USAJILI

 


HESABU ambazo zipo kwa sasa kwa kila timu ni kuona namna gani ambavyo zinaweza kukamilisha usajili kwa ajili ya msimu mpya wa 2021/22.


Sio kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara pekee bali ni mpaka Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili hakuna timu ambayo inalala kwa sasa macho yote ni kwenye usajili.


Tunaona kwamba moja ya timu ambayo inafanya usajili ule wa nguvu ni pamoja na DTB inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza. Hivyo hii inamaanisha kwamba kila timu ipo tayari kwa ajili ya msimu ujao.


Hata ambazo zimepanda Ligi Kuu Bara ikiwa ni Mbeya Kwanza pamoja na Geita Gold hawa wote wanapambana kuboresha vikosi vyao kwa ajili ya msimu mpya ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.


Hakuna namna ambacho kinahitajika kwa sasa ni benchi la ufundi kuachiwa mamlaka ya kufanya usajili na sio kuacha watu waingilie maamuzi yao ambayo wanayafanya.


Tuwakemee wale ambao wanaingilia maamuzi ya benchi la ufundi kwa sababu ikiwa wachezaji watasajiliwa bila kuwa ni pendekezo la mwalimu itakuwa kazi kubwa kuwatumia kwa wakati ujao.


Kinachohitajika ni kutumia ripoti ya mwalimu katika kufanya usajili na hii itasaidia msimu ujao kuwa na ushindani wa kweli na kila timu kuwa sawa kwa ajili ya kusaka ushindi.


Kwa sasa timu zote ambazo zinashiriki ligi zote ni timu kubwa na zinaweza kupata matokeo kwenye mechi zote ambazo watacheza kwa msimu ujao.


Jambo la msingi ni maandalizi mazuri na kufanya kila kitu kiwe kwa utaratibu ambao umepangwa na hilo litasaidia kuwa na mwendelezo mzuri.


Zipo timu ambazo zimekuwa zikishindwa kwenda na kasi mwanzo na kuamua kuchanganya pale inapofika mzunguko wa pili.


Hapo kuna tatizo ambalo limekuwa likiishi kwa muda mrefu lazima lifanyiwe kazi. Kikubwa ni kuona kwamba kuanzia mwanzo wa ligi mpaka mwisho ligi itakapoanza ushindani unakuwa mkubwa.


Hakuna tena neno la hii ni timu ndogo ambalo linapaswa kupewa nafasi kwenye akili za wachezaji pamoja na viongozi wa timu.


 Kila timu ni kubwa, zote zina kazi ya kusaka matokeo ili mwisho wa siku zipate ushindi. Hakuna maajabu katika kusaka ushindi bali lazima kuwe na maandalizi ambayo yanapaswa kuanza kufanyika kwa wakati huu.


Itazame Mwadui FC ambayo msimu ujao itashiriki Ligi Daraja la Kwanza. Kwenye mechi zake za mwisho ilizinduka na kuanza kucheza soka makini. Ila ilikuwa ilishachelewa mipango ikabuma na sasa ina kazi nyingine kwa ajili ya wakati ujao.

SOMA NA HII  POKEA SALAMU ZA MWAKA MPYA KUTOKA SOKA LA BONGO...HUU NI ZAIDI YA MWAKA KWAKO..UKO TAYARI..?


Haipaswi  kuwa na unyonge kwenye mechi ambazo zitachezwa msimu ujao ila kikubwa ni umakini kwa wakati huu hasa kwenye usajili na maandalizi hakuna namna nyingine.


Kwa zile ambazo bado hazijapokea ripoti itakuwa ni ajabu kuona kwamba hazijawakumbusha makocha wao kuweza kufanya hivyo. Ngoma ni nzito kwa sasa kwani dirisha la usajili linakaribia kufungwa.


Tubadilishiwe wimbo kwa wakati ujao kwamba wachezaji waliosajiliwa hawakuwa chaguo la mwalimu bali iletwe sababu nyingine tofauti na wimbo huu ambao unarudisha nyuma mafanikio yetu.


Ushindani ulikuwa mkubwa msimu uliopita hilo ni jambo ambalo linapaswa kuwa endelevu na hata msimu mpya wa 2021/22 utakapoanza.


Ikumbukwe kwamba kumekuwa na kasumba ya timu nyingi kuweka mtego kwamba mechi za mzunguko wa kwanza huwa wanazichukulia kawaida, hakuna yale mapambano ya kweli yanayoonekana.


Imekuwa kawaida kwamba pale wanapopoteza utaskia bado kuna mechi zinakuja mbele hivyo tuna nafasi ya kubaki ndani ya ligi.


Hizo mechi ambazo zinakuja zimekuwa zikiwapa presha na kufanya hata mpira wakitoa wao ukirushwa kwa timu pinzani wapeleke lawama kwa waamuzi wakidhani wanaonewa.


Hizi pia nazo kwa msimu mpya ziwekwe kando. Mapambano yaanze mzunguko wa kwanza na kila mmoja afanye kazi kwa juhudi kutimiza majukumu yake.


Kila timu ni bora na msimu mpya huwa unakuwa na mambo mengi. Kwa timu zote ni muhimu kujipanga vizuri na wachezaji kazi yao iwe kutimiza majukumu yao uwanjani.


Pia tumeona kwamba Kombe la Kagame limekwama kubaki ardhi ya Tanzania kwa kuwa wawakilishi wetu ambao ni KMKM, Yanga na Azam FC kushindwa kulipambania vema.  


Pia kwa wachezaji vijana ambao walipewa nafasi ni muhimu kutunzwa ili wakati ujao pia wapate nafasi ya kuweza kushiriki katika mashindano mengine pia.


Maumivu ya mashabiki kukosa Kombe la Kagame basi yahamishiwe kwenye furaha ya ligi itakapoanza huku ule usajili uwe ni ule uliofuata mapendekezo ya kocha.


Wakati mwingine ikitokea ni muhimu kwa wachezaji kupambana ili kuweza kufikia malengo ya kubakiza taji lolote ambalo litakuja kwenye ardhi ya Tanzania.


Hii itawafanya mashabiki wazidi kuwa na furaha kwa wale wachezaji ambao wanatimiza majukumu yao na inawezekana kila wakati kufanikiwa mipango hiyo kama wachezaji watajipanga na viongozi watajipanga pia.