MIAKA minne inatosha! Ndio kauli ya mchezaji wa zamani wa Yanga Allan Shomari ambaye amefunguka kutokana na usajili uliofanywa na timu hiyo anaamini msimu ujao lazima itatwaa ubingwa na kuondoa ukame wa miaka minne mfululizo bila ubingwa.
Mchezaji huyo ambaye kwa sasa ni mlemavu wa macho (kipofu) aliyasema hayo alipotembelewa na wanawachama wa Yanga mkoa wa Arusha nyumbani kwake Kisongo katika kuadhimisha Wiki ya Mwananchi hivi karibuni.
Akizungumzia msaada wa wanachama hao, aliwashukuru kwa mchango ambao wamekuwa wakimpa kwani ni ishara ya upendo na kumkumbuka na kuwaomba kumtembelea mara kwa mara bila kusubiri hadi kilele cha wiki ya Mwananchi.
“Timu yetu msimu huu ni nzuri nina asilimia zote lazima tutabeba ubingwa lakini vijana hapa nyumbani wazidishe juhudi kwani mambo yamebadilika hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanazingatia yote ya msingi ili wafike mbali,” alisema Shomari.
Mlezi wa Yanga mkoa wa Arusha, Shehe Maulid Hussein alisema walitumia siku hiyo kumkumbuka mchezaji huyo wa zamani ambaye alikuwa na msaada mkubwa kwa timu kipindi anacheza soka na kuongeza kuwa zoezi la kumtembelea itakuwa ni endelevu.
Alisema huo ni mwanzo tu kwa wana Yanga Arusha kwani anaamini matawi mengi yatajitokeza na kumshika mkono huku akimpa pole na kumtia moyo kwa kuwa maisha bado yanaendelea.