MOJA ya miamba wababe na wakorofi ndani ya uwanja ni pamoja na mshambuliaji wa kikosi cha AC Milan kwa sasa Zlatan Ibrahimovic.
Nyota huyo ambaye jezi yake ni namba 11 ni moja ya washambuliaji wakubwa duniani kutokana na uwezo wake na hali ya kujiamini muda wote awapo kazini.
Anatajwa kuwa na mabao mengi kibindoni ambayo ni zaidi ya 570 huku yakijumuisha mabao 500 katika ngazi ya klabu.
Pia mshambuliaji huyo anaingia katika orodha ya wachezaji ambao wamecheza timu nyingi duniani na kipaumbele chake kwa mabosi zake kila wakati huwa anawaambia wampe mkwanja mrefu yeye atafanya kazi ya kufunga kwa namna yoyote ile.
Timu yake ya awali ilikuwa ni Malmo FF ambayo pia alicheza zama zile za utoto na katika timu ya wakubwa alicheza msimu wa 1999/2001 na rekodi zinaonyesha kuwa alicheza jumla ya mechi 40 na kutupia mabao 16.
Waliwahi kuzinguana na nyota wa Chelsea kwa sasa Romelu Lukaku ndani ya uwanja zama hizo alipokuwa ndani ya Inter Milan huku Ibrahimovic akiwa na uzi wake wa AC Milan.
Maisha yake ndani ya Paris Saint German inaonekana aliyapenda kwa kuwa alicheza mechi nyingi kuliko klabu zote alizopitia ambapo ni mechi 122 na alitupia mabao 113 ilikuwa ni 2012/2016.
Kwa sasa amerejea AC Milan ambayo aliitumikia 2010/11 akiwa kwa mkopo akitokea Klabu ya Barcelona na alinunuliwa rasmi na AC Milan 2011/2012 na alipokuwa ndani ya Barcelona inayoshiriki La Liga alitupia jumla ya mabao 16 katika mechi 29.
Pia mwamba huyo alikipiga ndani ya kikosi cha Manchester United ilikuwa ni 2016/18 alicheza jumla ya mechi 33 na kutupia mabao 17.
Raia huyo wa Sweden akiwa na umri wa miaka 39 ana tuzo kibao kabatini mwake ambapo ni 14 za mchezaji bora wa mwaka, katika hizo ni mbili alizitwaa akiwa nchini Italia na 12 alizitwaa akiwa Sweden.
Ana tuzo tano za kuwa mfungaji bora ambapo alizotwaa na msimu wa 2015/16 alitupia mabao mengi ambayo ni 38 ndani ya Ligue 1 alipokuwa PSG, taji moja la Ligi Kuu England akiwa na Manchester United 2017 pia alishinda taji moja la Europa League akiwa na Manchester United.
Taji moja la FIFA Club World Cup ilikuwa ni 2010 akiwa na Barcelona, mataji manne ya Ligue 1 akiwa na PSG ni mataji kibao amenyanyua nyota huyo yanafika 31.