TIMU nne kwa sasa zina kazi ya kupeperusha bendera ya Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa hapo ni lazima wafanye kazi kubwa ili kupata matokeo chanya hakuna jambo lingine ambalo wanatakiwa kufanya.
Ni Azam FC na Biashara United hawa wapo kwenye upande wa Kombe la Shirikisho na wapo hatua ya kwanza kazi kubwa inatakiwa kufanyika kwao ili kuweza kusonga mbele.
Katika mechi zao za awali bahati njema kwao wote wawili wameweza kutusua na kupata ushindi katika hilo wanastahili pongezi.
Hawa ni Azam FC ambao walianza nyumbani na kupata ushindi huku Biashara United hawa walianza ugenini nao wakapenya katika kusepa na ushindi ugenini, safi na kazi nzuri.
Sasa kinachofuata ni kwenye mechi za marudio ambazo zitaamua nani atakuwa nani na kwa kuwa ni mpira lolote linaweza kutokea jambo la msingi ni kushikilia palepale ambapo mlinza awali.
Benchi la ufundi, wachezaji pamoja na viongozi kazi ni moja kuweza kufanya vizuri kwa kuendelea kushirikiana na kufanya kazi bila kuchoka kila wakati.Wawakilishi wote kimataifa komaeni.
Kwa upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika ni Yanga ambao walianza kufanya kazi mbele ya Rivers United ya Nigeria na mchezo huo uliochezwa bila ya mashabiki kama ilivyokuwa kwa Azam FC.
Ulikuwa ni mchezo mzuri kwa Yanga na mbaya kwa mashabiki kwa kuwa hakuna ambaye alitarajia kile kitatokea.
Kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 ni maumivu kwa mashabiki huku Yanga wao wakiwa kwenye nafasi nzuri ya kuona makosa yao na wanatakiwa kuyafanyia kazi ili waweze kushinda.
Wachezaji pamoja na benchi la ufundi hakuna haja ya kukata tamaa kwa muda huu kwa kuwa nafasi ipo ikiwa makosa yatafayiwa kazi.
Huu ni mpira na kila timu inastahili kushinda hivyo hakuna timu ambayo inapaswa kufungwa wala ambayo inapaswa kushinda muda wote.
Ikiwa hivyo basi isingekuwa na umuhimu wa kuwepo kwa mechi basi zile timu ambazo unadhani zinastahili kushinda zingekuwa zinakaa pembeni na kuziacha timu nyingine kushiriki. Kwa kuwa ni mpira basi ni lazima mchezo uchezwe.
Simba wao wanazali kwa kuwa walifanya vizuri msimu uliopita hawataanza kwenye hatua ya awali. Kazi kwao kwa sasa ni kufanya maandalizi zaidi kwa kuwa ukiwa mkubwa na wale ambao utakutana nao watakuwa wakubwa zaidi.
Mazoea ya kufikiria kwamba msimu uliopita tulifanya vizuri na msimu huu itakuwa vile yayeyuke kabisa kwenye akili za wachezaji pamoja na benchi la ufundi.
Kila mchezaji ajipe kazi ya kufanya, kila mmoja apambane kwa ajili ya bendera ya Tanzania na kuweza kuvunja rekodi ya msimu uliopita ya kutinga hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mtu ashinde kwa kutumia nguvu zake mwenyewe na hakuna ujanjaujanja ambao utafanyika kwani tunahitaji kuona kwamba kila kitu kinakwenda sawa.
Inawezekana na kila kitu kipo mikononi mwenu kwa sasa ni suala la kuamua kufanya vizuri na kupata matokeo. Ushindani wa kimataifa ni mgumu nanyi komaeni mfanye vizuri.