KOCHA mkuu wa Simba, Didier Gomes amesema mchezo wao wa kesho dhidi ya TP Mazembe ni sehemu mojawapo ya maandalizi kwa ajii ya mchezo wao wa Ngao ya hisani dhidi ya Yanga utakaochezwa Septemba 25 katika uwanja wa Mkapa.
Simba na Mazembe zitacheza kesho Septemba 18 kwenye kilele cha Tamasha la Simba Day litakalofanyika katika uwanja wa Mkapa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Gomes amesema mchezo huo ni mgumu kutokana na ukubwa wa wapinzani wao.
“Mechi ni ngumu kwa sababu Tp Mazembe ni timu kubwa Afrika na kipimo chetu sisi kwa ajili ya mchezo wetu wa wiki moja ijayo, tunashukuru wamekubali kuja,” amesema Gomes.
Gomes amesema anatambua ugumu wa mchezo huo huku wakiwa hawajawahi kupata ushindi wanapokutana.
“Tulicheza nao kwenye mashindano ya Simba na tulitoka nao sare, tunataka mchezo huu utupe nguvu zaidi kwa ajili ya kucheza Ligi vizuri pia,” amesema Gomes na kuongeza;
“Baada ya kucheza kwenye Ngao ya hisani tutakuwa pia na hesabu zingine kwa ajili ya Caf na mchezo huu wa Mazembe utatuonyesha vitu vingi.”
Nahodha wa Simba, John Bocco amesema mchezo huo ni mzuri na utawasaidia wao kupata nguvu ya kuingia katika msimu mpya.
“Mashabiki wajitokeze kuona kitu ambacho walimu wametutengeneza na kuwaonyesha katika uwanja, tunawaahidi wataona ubora zaidi ya misimu ya iliyopita.”