Home news KUELEKEA MECHI YA JUMAPILI DHIDI YA WANIGERIA…MUKOKO ASHUSHA PRESHA YANGA..NABI AFUNGUKA HAYA

KUELEKEA MECHI YA JUMAPILI DHIDI YA WANIGERIA…MUKOKO ASHUSHA PRESHA YANGA..NABI AFUNGUKA HAYA


KOCHA Nasreddine Nabi anaendelea kukinoa kikosi chake, lakini ameikuta kazi yake imefanywa nyepesi baada ya kuwa na uhakika kiungo wake mkabaji, Mukoko Tonombe kuwepo kwa ajili ya mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria.

Mukoko aliwapa presha mashabiki wa Yanga kutokana na kutokuwa fiti, kiasi hata kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki siku ya Kilele cha Wiki ya Mwananchi, alipwaya hadi akatolewa na Nabi wakati timu yake ikilala 2-1 dhidi ya Zanaco ya Zambia.

Hata hivyo, habari njema ni kwamba kiungo kutoka DR Congo kwa sasa yupo fiti kuwavaa Wanigeria, huku nyota wengine watatu wakiwamo mabeki wawili wa kushoto, Yassin Mustafa na David Brayson pamoja na winga Mapinduzi Balama waliokuwa majeruhi wa muda mrefu wakirejea.

Yanga inatarajia kuwa mwenyeji wa Rivers Jumapili hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, mchezo utakaopigwa kuanza saa 11 jioni, lakini itawakosa Mustafa, Balama na Bryson waliorejea chini ya uangalizi wa kocha wa viungo wa timu hiyo kuwekwa fiti zaidi, huku Mukoko akiwapunguza presha.

Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alilithibitisha kuwa nyota ambao wamebaki kwenye uangalizi na kocha wa viungo na watakosa mchezo wao wa awali ni Mustafa, Mapinduzi na Bryson huku akisisitiza kuwa Mukoko yuko fiti kuwavaa Wanigeria watakorudiana nao Septemba 19 nchini Nigeria.

Hafidh alisema ni wachezaji hao watatu tu ndio wana asilimia kubwa za kukosekana kwenye mchezo huo wa Jumapili, lakini habari njema ni kwamba Mukoko ambaye pia alianza kufanya mazoezi mepesi ili aweze kuwa fiti tayari amerudi kikosini na anaendelea vizuri chini ya kocha Nabi.

“Mukoko amekuwa fiti na yupo tayari kwa mchezo huo, ila hao wengine hawatakuwa kwenye mpango wa mwalimu hutokana na kutokuimarika vizuri, wanaendelea na mazoezi chini ya uangalizi,” alisema Hafidhi.

Tangu ajiunge na Yanga msimu uliopita kutoka As Vita ya kwao Congo, Mukoko amekuwa mmoja wa nyota tegemeo wa vijana wa Jangwani, ambapo kwa msimu uliopita aliifungia mabao matatu, huku akiwa kama injini ya timu na pale alipokosekana pengo lake lilionekana wazi.

SOMA NA HII  BAADA YA KUMSAJILI...YANGA WAFUNGUKA WALIVYOMPATA 'SURE BOY' USIKU USIKU..

Kwa sasa mwamba huyo kikosini ameletewa majembe mengine matata wa kumuongezea nguvu akiwamo Khalid Aucho kutoka Uganda na Yannick Bangala ambaye licha ya kuwa beki wa kati, lakini anamudu kucheza kama kiungo mkabaji kama alivyotumika siku ya Wiki ya Mwananchi pale alipompokea Mukoko.