WACHEZAJI waandamizi wa Azam, viungo Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya na beki Aggrey Morris wamesimamishwa na uongozi wa timu hiyo kwa muda usiojulikana huku wakishindwa kujua makosa yao.
Ni zaidi ya mwezi sasa tangu wachezaji hao wasimamishwe kufuatia kupewa barua ambazo zinadai wamesimamishwa kwa muda usiojulikana bila ya kuelezwa makosa yao.
Mmoja kati ya wachezaji hao ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, alisema kuwa mpaka sasa hawajui kwa nini wamesimamishwa kwa muda usiyojulikana kwa kuwa hakuna walipoelezwa makosa yao.
“Ni mwezi sasa tangu tusimamishwe na kifupi hakuna ambaye anajua kati yetu ni kwa nini labda tumesimamishwa yaani unavyoona huko mitandaoni watu wakiongea na sisi tunaona hivyo hivyo hatujui chochote na hakuna ambaye kati yetu anajua sababu ya kusimamishwa kwa muda usiojulikana,” alisema mchezaji huyo.
Championi lilimtafuta ofisa habari wa timu hiyo, Thabith Zakaria ‘Zaka Zakazi’ lakini hakuweza kupatikana kutokana na simu yake kuita muda mrefu bila ya kupokelewa.