WAKATI timu yake ya taifa ya Ufaransa ikifanikiwa kutwaa taji la UEFA Nations League kwa mara ya kwanza katika historia nyota Paul Pogba bado ni wa moto katika rekodi akiwa uwanjani katika mechi za Premier League.
Ikumbukwe kwamba Ufaransa ilitwaa taji hilo baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Hispania ambapo mabao yalifungwa na Kylian Mbappe pamoja na Karim Benzema na Pogba pia alikuwa sehemu ya kikosi cha ushindi.
Kiungo huyo mwenye miaka 28 aliletwa duniani Machi 15, 1993 anapenda kuvaa jezi namba 6 akiwa na timu yake ya Manchester United inayonolewa na Kocha Mkuu, Ole Gunnar Solskjaer.
Mpaka sasa ndani ya Manchester United ambapo aliibukia hapo 2016 akitokea Klabu ya Juventus amecheza jumla ya mechi 144 za ushindani.
Alipokuwa Juventus msimu wa 2012/2016 aliweza kucheza jumla ya mechi 124 na alitupia mabao 28 kama umri wake wa sasa.
Weka kando ishu za Juventus sasa tunarudi katika Klabu ya Manchester United ambapo yupo kwa sasa huku dili lake nalo likizidi kuyeyuka taratibu na anatajwa kuingia kwenye rada za Real Madrid.
Katika mechi 144 ambazo amecheza ametupia pia mabao 28 na pasi alizotoa ni 36 ametengeneza nafasi za wazi 27 pia amekosa nafasi za wazi kufunga 28.
Hivyo kama angefanikiwa kufunga katika kila nafasi ambazo alizipata hizo za wazi mwamba angekuwa ametupia jumla ya mabao 56 kibindoni ila hakuwa na bahati mabao yake yatabaki kuwa 28.
Rekodi zinaonyesha kwamba amepiga jumla ya pasi 8,785 ikiwa ni wastani wa pasi 61 katika kila mechi na hizi ni rekodi za Premier League pekee.