Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametaka Wizara ya Sanaa, Michezo na Utamaduni kuhakikisha timu ya Biashara United inasafiri kwenda Libya kwa ajili ya kucheza mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika siku ya Jumamosi
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa tuzo za Ligi Kuu msimu uliopita inayoendelea usiku huu, Waziri Mkuu amesema itakuwa jambo la kushangaza kuona Biashara United haijaenda Libya kwa ajili ya mechi hiyo ya marudiano
“Mkurugenzi Baada ya shughuli hizi mkae mjipange biashara iondoke nchini na tunaamini watashinda. Timu iende ikashindwe huko lakini naamini itashinda. Mhakikishe timu inaenda kule Libya,” alisema Waziri Mkuu
Waziri Mkuu Majaliwa alisema hilo litachochea ushindani katika Ligi Kuu kwani timu zitapata ari na moyo wa kupambana kupata nafasi ya kuwakilisha nchi kimataifa
Katika mchezo huo wa marudiano, utakaochezwa jijini Benghazi, Jumamosi jioni, Biashara United inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote ili iweze kutinga hatua ya mwisho ya mchujo ya mashindano hayo
Katika mchezo wa kwanza hapa Dar es Salaam, Biashara United iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Deogratias Mafie na Atupele Green