KIUNGO mchezeshaji hivi sasa tegemeo Simba, Mzambia, Rally Bwalya, amechaguliwa kuwa mpiga penalti maalum katika kikosi cha Thiery Hitimana.
Kiungo huyo ameonekana kuwa tegemeo katika timu hiyo akifunga mabao mawili katika michezo ya mashindano ambayo ni ule wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneg Galaxy na ule wa Ligi Kuu Bara waliocheza na Polisi Tanzania.
Awali, nahodha na mshambuliaji tegemeo wa timu hiyo, John Bocco ndiye alikuwa na jukumu hilo la kupiga kila penalti inapotokea akiwepo uwanjani.
Mmoja wa viongozi wa Benchi la Ufundi la timu hiyo, ameliambia Championi Ijumaa kuwa wachezaji wenyewe wamekubaliana na kumchagua Bwalya kupiga penalti zote akiwa uwanjani.
Kiongozi huyo alisema kuwa Bocco amechaguliwa kupiga penalti hizo kutokana na kufanya vizuri mazoezini kabla ya juzi kuanza jukumu hilo katika mchezo dhidi ya Polisi Tanzania uliomalizikakwa Simba kushinda bao 1-0 likifungwa na kiungo huyo kwa njia ya penalti.
Aliongeza kuwa baada ya wachezaji hao kumchagua Bwalya katika majukumu hayo, Hitimana alipitisha maamuzi hayo ya wachezaji hao.
“Hauwezi kuwataja wachezaji tegemeo hivi sasa wa Simba bila ya kumtaja Bwalya baada ya kuondoka kwa Luis (Miquissone) na Chama (Clatous).
“Bwalya anaibeba timu kutokana na mchango mkubwa anaoutoa katika mechi, baada ya kufunga mabao mawili ya mashindano katika ligi, jana (juzi) dhidi ya Polisi na mchezo wa marudiano wa kimataifa dhidi ya Galaxy.“
Licha ya kuwa tegemeo hivi sasa, kiungo huyo ameongezewa majukumu mengine mapya ya kupiga penalti kila anapokuwa uwanjani baada ya kuchaguliwa na wachezaji wenzake,” alisema kiongozi huyo.
Hitimana alithibitisha hilo kwa kusema: “Bwalya anafanya vizuri mazoezini katika upigaji wa penalti, sifa yake kubwa ni mtulivu, hana papara, hivyo ataendelea kupiga kila anapokuwa uwanjani.”