Home CAF MAMBO YA MSUVA HUKO MOROCCO NI ‘BULIBUL’….AZIDI ‘KUKIWASHA’ KADRI AJISIKIAVYO…

MAMBO YA MSUVA HUKO MOROCCO NI ‘BULIBUL’….AZIDI ‘KUKIWASHA’ KADRI AJISIKIAVYO…


MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva ameisaidia timu ya Wydad Casablanca kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku akitupia mabao mawili miamba hiyo ya Morocco ikiibuka na ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Hearts of Oak ya Ghana.

Katika mchezo huo wa marudiano, Wydad wakiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Mohammed V walikuwa na kibarua cha kupindua matokeo ya bao 1-0 ambalo walifungwa kwenye mchezo wa kwanza ugenini huko Accra, Ghana.

Msuva ndiye aliyefungua akaunti ya mabao kwa Wydad ikiwa ni dakika ya tano ya mchezo kabla ya kushuhudiwa yakifungwa mabao mengine matatu kabla ya mapumziko. Mabao hayo yalifungwa na Ayman El Hassouni, Achraf Dari na Yahya Jabrane kwa penalti.

Wydad walionekana kuwa na njaa ya mabao kwani baada ya kurejea kipindi cha pili walilisakama lango la wapinzani wao na kupata bao la tano lililofungwa na Ayoub El Amloud kabla ya Msuva kupiga bao la sita na la pili kwake kwenye mchezo huo dakika ya 61.

Mara baada ya mchezo huo, Msuva alisema haikuwa kazi nyepesi kutinga hatua ya makundi kwa mara nyingine kutokana na upinzani ambao wameupata kutoka kwa wapinzani wao ambao msimu uliopita walitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Ghana na Kombe la FA nchini humo.

“Tumeitumia vizuri faida ya kucheza nyumbani. Tulijiandaa vizuri na mchezo na tulitambua ugumu wake, lakini ilitubidi kuweka nguvu na akili zetu zote ili kuvuka kikwazo kilichokuwapo mbele yetu maana lengo ni kuchukua ubingwa wa Afrika,” alisema Msuva.

Akizungumzia mabao yake aliyopachika, alisema: ”Yalitokana na ushirikiano mzuri na wachezaji wenzangu. Sifa inabidi ziwaendee maana bila wao pengine nisingefunga, najiona mwenye furaha na nina imani hiki ambacho nimekifanya kwenye mchezo huu kitaendelea hata kwenye hatua ya makundi.”

Kwa misimu miwili iliyopita – 2019/20 na 2020/21 Wydad waliishia nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi Afrika kwa ngazi ya klabu.

SOMA NA HII  TIMU YA WIKI CAF...SIMBA SC WAWILI...KAPOMBE NA CHAMA NDANI