Home Makala MDAMU WA POLISI TANZANIA ANAAMINI ATAREJEA UWANJANI,AWASHUKURU WOTE

MDAMU WA POLISI TANZANIA ANAAMINI ATAREJEA UWANJANI,AWASHUKURU WOTE


GERALD Mathias Mdamu, ni mshambuliaji wa Polisi Tanzania ambaye alivunjika miguu miwili katika ajali waliyoipata timu hiyo ilipokuwa ikitoka mazoezini asubuhi ya Julai 9, mwaka huu.

Alipata matibabu kwenye Hospitali ya KCMC iliyopo Moshi, Kilimanjaro, kabla ya kuhamishiwa Muhimbili, Dar ambapo hivi sasa amepata ruhusa ya kurejea nyumbani.

Spoti Xtra limemtembelea mchezaji huyo nyumbani kwake ili kufahamu maendeleo yake mara baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali. Katika mahojiano haya, amefunguka masuala mengi ikiwemo hali yake kwa sasa na mazingira ya ajali ilivyokuwa.

MAZINGIRA YA AJALI

“Unajua ilipotokea ajali nilikuwa nimesimama mbele pale mlangoni, kwa hiyo nilibanwa na mti baada ya gari kugonga mti, ndio maana nilipata majeraha makubwa tofauti na wenzangu.


“Baada ya hapo nilipoteza fahamu, sikuwa nakumbuka kitu chochote ila baadae nilisimuliwa kuwa nilivyofika hospitali nilikuwa nasumbua sana kama nilikuwa nimechanganyikiwa, wakawa wananizuia.


HUDUMA KUTOKA KWA POLISI TANZANIA

“Kwa sasa Polisi wananihudumia vizuri kama kukiwa na tatizo lolote, pia mshahara wangu ninaupata kama kawaida.


“Mara ya mwisho walikuja nikiwa hospitali ila baadaye walishindwa kwa sababu kilikuwa kipindi cha usajili na timu ilikuwa inafanya maandalizi ya msimu mpya ambapo waliweka kambi mkoani Mwanza.

RUHUSA YA MADAKTARI

“Madaktari wa Muhimbili waliokuwa wananitibu waliniangalia hali yangu ilivyokuwa inaendelea na wakaniruhusu niende nyumbani, unajua nilikaa hospitali kwa muda mrefu jambo ambalo linachosha hata kwa mgonjwa, nimeathirika kisaikolojia, nilikonda sana, halafu nilikuwa sijazoea mazingira.

 

“Kila baada ya wiki mbili narudi Muhimbili kwa ajili ya kuangaliwa kama daktari wangu niliyenaye ananisafisha vizuri au vipi.

 

“Pia nimeambiwa nikirudi tena Muhimbili watanipiga X-Ray kwa ajili ya kuona mishipa inaendeleaje na nitarejea uwanjani baada ya muda gani.

 

“Mara ya kwanza nilienda hospitali hawakutoa vyuma, kwa hiyo hawajanisafisha ila niliandikiwa tarehe ya kurudi na kaka yangu ndio anayo yale makaratasi.

 


KUREJEA UWANJANI


“Kwa upande wangu nikijiangalia nasema nitarudi uwanjani ila madaktari ndio wataniambia kama nina uwezo wa kurudi baada ya kufanyiwa hiyo X-Ray.

SOMA NA HII  SUALA LA UWANJA WA FAINALI YA FA ITAZAMWE KWA UMAKINI

 

“Mimi ni mchezaji, nina malengo yangu, hivyo nikirudi najua sitakuwa kwenye ule ubora ambao nilikuwa nao mwanzo, ila nitaanza mazoezi polepole mpaka nitakaporudi kama mwanzo.

 

“Nina uhakika nitarudi taratibu maana nikisema nitarudi kama mwanzo nitakuwa muongo ila Mungu akinijalia nitakuwa zaidi ya pale nilipoishia, nitaipambania timu yangu kadiri ya uwezo wangu.

 

MAZUNGUMZO NA YANGA


“Mwanzo nilikuwa nimeanza mazungumzo na Yanga kwa ajili ya kujiunga nao kwa msimu huu ila baadaye tulikuja tukakatisha maongezi na ilikuwa kabla ya ajali kwani nilikuwa na mkataba wa mwaka mmoja Polisi, hivyo niliwaambia waongee na Polisi kwa ajili ya kuvunja mkataba.

 

SHUKRANI KWA WATANZANIA


“Fedha nilizochangiwa na baadhi ya watu kwa ajili ya matibabu nilizipata, nawashukuru sana Watanzania kwa ajili ya kunisaidia, wao ni wanadamu na wameguswa na tatizo langu.

 

“Wachezaji kwa sasa hivi hawaji kwa sababu wapo kwenye kazi zao ila mwanzo walikuwa wanakuja kunisalimia.

 

“Nawashukuru sana viongozi wa Polisi, wachezaji wenzangu na Watanzania wote ambao walikuwa na mimi tangu nimeanza kuumwa mpaka leo hii kwa kutambua kipaji changu na kunichangia michango mbalimbali, mpaka leo wanapigia simu kwa ajili ya kujua maendeleo yangu.

 

USHAURI KWA POLISI TANZANIA


“Sahivi ligi ni ngumu, ningewaomba wachezaji wenzangu wa Polisi wapambane kwa ajili ya kuisaidia timu ifanye vizuri na tufanikiwe msimu ujao kucheza michuano ya kimataifa kwani wenzetu waliocheza wanasema yana faida.

 

“Hivyo basi tusiangalie Simba, Yanga na Azam, sisi tuna uwezo wa kushika nafasi ya tatu kwenye ligi, nawaomba tupambane, najua tuna malengo makubwa.

 

“Nimeangalia mchezo dhidi ya KMC, nimeona wachezaji wenzangu wanapambana sana, hivyo waendelee kupambana zaidi ili tutimize malengo yetu,” anasema Mdamu.