Home news NABI AFUNGUKA TATIZO LA WACHEZAJI YANGA KUKOSA PUMZI KIPINDI CHA PILI..ADAI NI...

NABI AFUNGUKA TATIZO LA WACHEZAJI YANGA KUKOSA PUMZI KIPINDI CHA PILI..ADAI NI MBINU


LICHA ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMC FC Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amesema wachezaji wake hawakuishiwa pumzi kipindi cha pili kwenye mechi dhidi ya KMC, bali ilikuwa ni mbinu baada ya kupata mabao mawili ya haraka.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mechi ya raundi ya tatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kupata ushindi wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea mkoani Ruvuma, Nabi kupitia kwa Msaidizi wake, Cedric Kaze raia wa Burundi, alisema hakukuwa na ulazima wowote wa kuendelea kukimbizana kwani tayari walikuwa wameshapata mabao mawili, hivyo kazi iliyobaki ilikuwa ni kuyalinda tu.

“Tumeshafunga mabao mawili dakika 15 za mwanzo, ilikuwa ni lazima tutulie, kwanza tupo ugenini, tuliocheza nao ndiyo walitakiwa kuwa na presha na sio sisi, si kweli kusema eti pumzi imepungua, hata ukifanya tathmini, sisi ndiyo tuliomiliki zaidi,” alisema.

Wachambuzi na wataalamu wa masuala ya soka, wanadai kuwa wachezaji wa Yanga huanza kwa kwa kasi, lakini huanza kupungua taratibu kadri muda unavyozidi kwenda na hii yote inaonekana kuwa wanaishiwa pumzi, hasa kuanzia dakika ya 60.

Msimu huu, Yanga haijawahi kufunga bao kipindi cha pili, ingawa pia haijaruhusu bao lolote kuanzia mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, hadi mechi tatu za Ligi Kuu.

Kaimu Kocha wa KMC, Hamad Ally, alisema wamepoteza mechi hiyo kutokana na umakini hasa kipindi cha kwanza.

“Tulifanya makosa kipindi cha kwanza, lakini kipindi cha pili tulibadilika na kupata nafasi ambazo hatukuzitumia na hilo tutakwenda kulifanyia kazi.

Wakati huo huko, kipa wa KMC, Farouk Shikalo, amesema walifungwa na Yanga, baada ya kuzidiwa eneo la katikati hasa kipindi cha kwanza.

“Walimiliki katikati, unajua Yanga ni timu kubwa na ina wachezaji wazoefu, wakatuwahi, mimi peke yangu nisingeweza kuzuia, walipata nafasi zile wakatufunga, baadaye tulipojirekebisha walikuwa tayari wanaongoza kwa mabao mawili,” alisema kipa huyo ambaye msimu uliopita aliichezea Yanga.

SOMA NA HII  KWA KAULI HII YA KITASA KIPYA CHA JANGWANI....MASHABIKI YANGA MSIPOANGALI MTAUMWA KISUKARI...

Yalikuwa ni mabao ya Fiston Mayele likiwa ni la kwanza kwake kwenye Ligi Kuu msimu huu na Feisal Salum ambaye ni bao lake la pili, moja akilifunga kwenye mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar, Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

Yanga ambayo ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi tisa baada ya michezo mitatu, itashuka tena dimbani Oktoba 30, mwaka huu kuikaribisha Azam FC katika mechi itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.