Home news RASMI…SIMBA WAAMUA KUIPOTEZEA MICHUANO YA CAF…HITIMANA ATOA MSIMAMO…

RASMI…SIMBA WAAMUA KUIPOTEZEA MICHUANO YA CAF…HITIMANA ATOA MSIMAMO…


LICHA ya kuendelea kuwapo katika mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba ya jijini Dar es Salaam wamesema kwa sasa kipaumbele chao ni kuona wanatetea ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ambao wanaushikilia.

Kauli hiyo ya Simba imetolewa baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara dhidi ya Polisi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi.

Jumapili iliyopita Simba ilitolewa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Jwaneng Galaxy ya Botswana na sasa itacheza mechi ya mtoano na Reds Arrows ya Zambia ambapo mshindi atatinga hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Akizungumza  jana, Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Thierry Hitimana, alisema wameamua kuweka nguvu kwenye mechi za Ligi Kuu kwa sababu wanahitaji kutwaa ubingwa kwa mara ya tano mfululizo na wameweka kando mikakati ya mchezo wao dhidi ya Red Arrows.

Hitimana alisema nguvu na akili zao zote zitakuwa katika kutafuta pointi tatu kwenye kila mechi ya Ligi Kuu Tanzania na si kitu kingine.

“Tumeona ratiba na tumemfahamu mpinzani wetu tutakayekutana naye katika Kombe la Shirikisho, hatuwezi kusema lolote kuhusu Reds Arrows kwa sababu mechi iko mbali, kipaumbele chetu ni Ligi Kuu,” alisema Hitimana.

Aliongeza hawezi kuanza kuufikiria mchezo huo kwa sababu bado ana mechi nyingine mbili ‘ngumu’ ambazo ni dhidi ya Coastal Union na Ruvu Shooting ambazo wanahitaji kuondoka na pointi zote sita katika michezo hiyo.

“Kwa sasa hatuwezi kuizungumzia Reds Arrows kwa sababu tuna kibarua kigumu mbele yetu kuhakikisha tunashinda mechi za ligi kuu zilizopo mbele yetu ikiwamo dhidi ya Coastal Union na Ruvu Shooting ambazo ziko karibu.”

“Tunatambua ligi msimu huu kuna ushindani mkubwa, tumerejea uwanjani kufanyia kazi madhaifu yetu yaliyotokea katika michezo iliyopita ikiwamo tuliocheza jana (juzi ) dhidi ya Polisi Tanzania,” alisema Hitimana.

Aliongeza malengo makubwa ya Simba ni kufanya vizuri katika michezo yote iliyopo mbele yao na itakapokaribia mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika wataanza maandalizi yake.

SOMA NA HII  PAMOJA NA USHINDI WA JUZI....MAKI KATAZAMA MASTAA WAKE WEEH....KISHA AKATIKISA KICHWA KUKATAA UWEZO WAO...

Kuhusu mechi ya juzi, Hitimana alisema walicheza kwa ‘presha kubwa’ iliyotokana na ‘mawenge’ waliyokuwa nayo baada ya kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Ningependa kuwapongeza na kuwashukuru wachezaji wangu kwa kupambana na kupata pointi tatu muhimu. Katika mchezo wa jana (juzi), tulikuwa na wapinzani wawili, wa kwanza ni sisi wenyewe pamoja na Polisi Tanzania, kikubwa tumepata ushindi na kufikia malengo katika mchezo huu,” alisema kocha huyo.

Alisema mabadiliko ya wachezaji wanne katika kikosi kilichoanza juzi yalitokana na baadhi ya nyota wake wanaocheza katika eneo la kiungo kuwa majeruhi na ndio maana alibadilisha kikosi.

“Ukiangalia Taddeo Lwanga ni majeruhi aliumia kwenye mechi dhidi ya Jwaneng Galaxy, na Jonas Mkude hakuwa fiti asilimia 100 ndio maana tumefanya mabadiliko yale kikosini ingawa nilitamani kuanza na washambuliaji wawili, lakini kikubwa tunafurahi kwa ushindi tuliopata,” kocha huyo alisema.

Simba inaendelea na mazoezi kwa ajili ya kuwakaribisha Coastal Union katika mechi nyingine ya Ligi Kuu itakayochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini.