Home Habari za michezo LIGI KUU BARA 2023/24 MACHO YOTE KWA MAKOCHA, YANGA NA KOCHA WAO...

LIGI KUU BARA 2023/24 MACHO YOTE KWA MAKOCHA, YANGA NA KOCHA WAO MPYA SASA

Habari za Yanga

WAKATI Ligi Kuu Bara ikitarajiwa kuanza mwezi ujao, timu mbalimbali zimefanya mabadiliko ya benchi la ufundi kwa lengo la kutaka mapinduzi mapya ya kufanya vizuri na wengine wakisaka mkono mrefu zaidi kwingine.

YANGA
Yanga imemsajili Kocha Miguel Gamondi akichukua mikoba ya aliyekuwepo Nasreddine Nabi ambaye baada ya kuipa klabu hiyo mafanikio kwa misimu miwili mfululizo aliamua kutimka kusaka changamoto nyingine.

Jicho la wengi litamfuatilia kocha mpya, watu watataka kuona ni kitu gani ambacho anacho? Je, atakuja na mfumo gani ambao wachezaji wataushika na kumsaidia kupata matokeo katika mechi mbalimbali za mashindano ya Ligi Kuu na kimataifa.

Gamondi ambaye ni raia wa Argentina ni kocha mwenye uzoefu na soka la Afrika kwa sababu ameshawahi kufundisha klabu kubwa zikiwemo Wydad Casablanca ya Morocco, Mamelod Sundown na Platnum Stars za Afrika Kusini, CR Belouizdad na nyingine nyingi.

Ni mara ya kwanza atafundisha kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, ambayo inatajwa kama
miongoni mwa ligi ngumu. Mfumo anaotumia kocha huyo ni 4-2-3-1. Je, mfumo huo utamwezesha kupata matokeo?

Kwa sababu kocha aliyepita alikuwa anabadilisha mifumo tofauti kulingana na mechi anayokutana nayo. Bila shaka mashabiki na wadau wa soka watamfuatilia mara ligi itakapoanza kuona upi ubunifu wake na udhaifu wake katika kupanga kikosi kitakachompa
ushindi kwa kila mchezo.

AZAM FC
Klabu ya Azam FC ina kocha mpya Youssouph Dabo aliyechukua nafasi za waliokuwepo; Daniel Cadena na Kally Ongalla. Dabo raia wa Senegal anatarajiwa kuipa Azam mafanikio katika mechi za Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.

Kwa muda mrefu Azam FC imeshindwa kutamba nyumbani na hata kimataifa huenda usajili wa kocha huyo ulioenda sambamba na baadhi ya wachezaji wapya utasaidia kufikisha malengo waliyojiwekea.

Dabo anatua kwenye timu hiyo baada ya kuachana na ASC Jaraaf de Dakar huku akikumbukwa zaidi baada ya kuifundisha Teungueth iliyokuwa na staa wa Simba, Pape Sakho na Malikcou Ndoye wa Azam.

Dabo mwaka 2016 akiwa na Teungueth alitwaa ubingwa wa Kombe la Ligi na 2017 akiwa Kocha wa Teungueth alifika fainali ya Kombe la Senegal (sawa na Kombe la Shirikisho la
Azam hapa nchini).

Pia, aliwahi kufundisha timu za vijana za taifa hilo kwa mafanikio makubwa hivyo uzoefu alionao hakika ataisaidia Azam FC kama inavyotarajiwa. Jicho la mashabiki na wadau wa soka lazima litamuangazia kuona ataiweza Ligi Kuu?

Ukiachana na klabu hizi kubwa, timu nyingine ni kama zimechukua makocha ambao ni wazoefu wakitoka huku na kuingia kule.

NAMUNGO
Namungo imemtangaza Cedric Kaze kuwa kocha wao mkuu. Aliwahi kuifundisha Yanga msimu wa mwaka juzi kisha akatimuliwa na kurudi kama kocha msaidizi akisaidiana na Nabi ambao waliisaidia Yanga kutimiza malengo kwa kufanya vizuri.

Kaze tayari ana uzoefu na ligi ya Tanzania hivyo anategemewa kuipa mafanikio timu hiyo ambayo msimu uliopita hawakufanya vizuri sana.

GEITA GOLD
Geita Gold imemchukua Kocha Hemed Morocco kuziba nafasi ya aliyekuwepo Fred Minziro waliyeachana naye.

Morocco ni kocha mzoefu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na ile ya Zanzibar kwani amewahi kufundisha klabu mbalimbali kama Namungo, Singida, KMKM, timu za taifa Zanzibar na Tanzania.

PRISONS
Tanzania Prisons imemtangaza Kocha Fred Minziro kuwa kocha wao mpya akichukua nafasi ya Abdallah Mohamed. Kwa misimu miwili mfululizo timu hiyo imekuwa ikifanya vibaya hadi dakika za mwisho ikionekana kupambana kutoshuka daraja.

Huenda Minziro kwa sababu ya uzoefu wake wa muda mrefu akaisaidia timu hiyo msimu huu kufanya vizuri.

COASTAL
Coastal Union imemtangaza kocha Mwinyi Zahera kuwa kocha wao mpya akitarajiwa kuisaidia timu hiyo msimu huu baada ya kuyumba zaidi msimu uliopita.

Zahera anabebwa na uzoefu wake kwenye ligi ya Tanzania baada ya kuwahi kuzifundisha Yanga, Polisi Tanzania na sasa anatazamiwa huenda atakuja na mbinu nyingine za kuifanya timu hiyo kung’ara.

Msimu uliopita Coastal Union ilifundishwa na Fikiri Elias ambaye ameshindwa kuipa timu hiyo mafanikio kama ilivyokusudiwa.

KMC

KMC imemtangaza kocha Abdihamid Moallin kwa ajili ya msimu huu akichukua nafasi ya Hitimana Thierry na Habibu Kondo ambao walishindwa kuendana na ushindani msimu uliopita.

Moallin aliwahi kuifundisha Azam FC msimu wa mwaka jana na baadaye wakaachana naye baada ya kushindwa kufanya vizuri kama ilivyotarajiwa. Baada ya kupata uzoefu wa soka la
Tanzania inatarajiwa kuisaidia timu hiyo kufikisha malengo iliyojiwekea.

MTIBWA SUGAR
Wakata miwa wa Morogoro, Mtibwa Sugar nao hawakuwa nyuma kufanya mabadiliko
wamemchukua Habibu Kondo kuwa Kocha Mkuu. Kondo anachukua nafasi ya Salum Mayanga aliyemalizana na timu hiyo msimu uliopita.

Kondo ni kocha mwenye uzoefu aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwemo KMC, Stand United na nyingine. Huenda kocha huyo akairejesha Mtibwa kwenye kiwango kwa sababu katika misimu miwili mfululizo imekuwa ikicheza kwa presha kila mwishoni mwa msimu.

Hao ni baadhi tu ya makocha ambao wamesajiliwa na pengine watatazamwa wamekuja na nini kwenye timu zao katika kuzipa mafanikio.

Watakuwa kwenye presha kubwa kwa sababu wanahitaji kufanya kitu ambacho wenzao waliotemwa hawakukifanya au kuendeleza yale mazuri.

SOMA NA HII  KUELEKEA KARIAKOO DABI....MO DEWJI AMFUNIKA VIBAYA MNOO GSM...AWEKA MEZANI MIL 500 CASH...