Home Habari za michezo SIMBA SC WASHTUKIA MCHEZO M’BAYA KWA INONGA…WAMPIGA STOP FASTA…

SIMBA SC WASHTUKIA MCHEZO M’BAYA KWA INONGA…WAMPIGA STOP FASTA…

Habari za Simba SC

Wakati mabosi wa Simba SC wakiwa kwenye harakati za kuboresha kikosi chao katika dirisha hili dogo la usajili kuna wachezaji watatu hadi sasa ni suala la muda tu kutua ndani ya timu hiyo, lakini wakisema Henock Inonga haondoki kwa sasa.

Wakati hilo likiendelea Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema hakuna mchezaji yeyote anayetoa mchango wa kutosha kwenye timu na akaondoka hata kama mkataba wake unakwenda ukingoni mwishoni mwa msimu huu.

Try Again alisema kwenye hili dirisha dogo la usajili wataongeza wachezaji wachache wapya kulingana na upungufu wa kikosi chao kwenye maeneo tofauti kama ilivyoonekana katika mzunguko wa kwanza.

Alisema uongozi wa Simba SC utakwenda sokoni kuwatafuta wachezaji bora baada ya benchi la ufundi na wataalamu wao kutoka kwenye maeneo tofauti wakiwa wamejadiliana kwa pamoja na kukubaliana.

“Baada ya kulimaliza hilo, tunaendelea na michezo ya mzunguko wa pili wale wachezaji wanaomaliza mikataba mwishoni mwa msimu kama, Inonga hatakwenda kokote zaidi ya kuboreshewa mikataba mipya na kubaki hapahapa, huwezi kumuacha mchezaji mzuri akaondoka kwenye timu,” alisema Try Again na kuongeza;

“Uongozi, benchi la ufundi tumekubaliana kutengeneza timu imara zaidi ya iliyopo ndio maana tupo sokoni kutafuta wachezaji wazuri baada ya hapo tutawabakiza nyota wetu muhimu kabla ya mikataba yao kufikia ukingoni tutakuwa tumewaongeza mipya tayari.

“Unajua misimu miwili nyuma tuliwauza nyota wetu imara wa kikosi cha kwanza, Luis Miquissone na Clatous Chama baada ya kuondoka timu ilipitia wakati mgumu, hatutafanya makosa kama hayo tena.

“Tunaendelea na mambo hayo mawili kwa utulivu mkubwa ili kusuka timu bora kwenye mashindano ya ndani pamoja na yale ya CAF, kwa kuwa na wachezaji wenye viwango bora.”

Mbali na Inonga pia Sadio Kanoute ambaye amekuwa kwenye ubora wa hali ya juu mkataba wake umebakiza miezi sita tu, hivyo mwishoni mwa msimu atakuwa mchezaji huru.

Hivi karibuni ilielezwa kuwa Yanga ilikuwa inamhitaji Inonga, lakini taarifa zikasema pia kuwa amegoma kusaini mkataba mpya akitaka kuondoka kwenda nje ya nchi ikiwa ni baada ya kuonyesha kiwango bora kwa kipindi chote alichokaa Simba.

Wachezaji wengine ambao mikataba yao inamalizika ni nahodha, John Bocco, Jonas Mkude, Erasto Nyoni na Benno Kakolanya ambao mwishoni mwa msimu huu lolote linaweza kutokea kwa upande wao kama watakuwa hajaongezewa mwingine.

SOMA NA HII  KUHUSU ISHU YA KUPISHA USAJILI MPYA....MIQUISSONE AWADINDIA MABOSI SIMBA....