ALIYEKUWA Kocha mkuu wa Simba, Didier Gomes wa Simba amefichua kuwa kiungo wa Yanga Feisal Salum ‘Fei Toto’ hana muda mrefu kabla hajasepa ndani ya timu hiyo.
Kocha huo aliyesitisha kibarua chake Msimbazi, amesema anamuona Fei Toto akienda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi katika klabu kubwa kutokana na kipaji kikubwa cha soka alichonacho.
Gomes aliyasema hayo alipofanya mahojiano maalumu na gazeti la Mwanaspoti baada ya kuafikiana na mabosi wa Msimbazi kuachia ngazi kuifundisha timu hiyo ilipotolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa mabao 3-1 na Jwaneng Galaxy ya Botswana, matokeo ya jumla kuwa 3-3 kuifanya timu itolewe kwa faida ya bao la ugenini.
Kocha huyo raia wa Ufaransa, alisema kwa namna anavyomuona Fei Toto na muda ambao amekaa nchini, mchezaji huyo hana muda mrefu wa kucheza soka katika Ligi ya Bara, kwani anaamini ana uwezo wa kukipiga nje ya nchi ikiwamo Ulaya.
“Feisal (Fei Toto) ni mchezaji mzuri sana, nimemfuatilia kwenye ligi na hata tulipokuwa tunakutana naye alikuwa anatupa wakati mgumu. Nadhani hana muda mrefu wa kuendelea kucheza hapa, ataondoka na kwenda kucheza ligi kubwa nje,” alisema Gomes.
“Kuna muda hata mimi nilitamani siku moja nifanye naye kazi nikiwa Simba, lakini nilikuwa nafahamu ni ngumu.”
Hii sio mara ya kwanza kwa kocha huyo kumuongelea Fei Toto, kwani aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Emmanuel Amunike aliwahi kukaririwa akisema mchezaji huyo anaweza kucheza Barcelona.
Kocha wa Simba misimu miwili iliyopita, Sven Vandenbroeck aliwahi kusema mchezaji huyo anapokuwa uwanjani ni hatari kutokana na mikimbio yake na kuwazidi ujanja viungo.
Fei amejihakikishia namba katika kikosi cha Yanga kwa misimu mitatu akiwa kama kiungo na msimu huu licha ya kutumika kama mshambuliaji wa pili (Namba 10) bado ameendelea kufanya vizuri.
Kocha wa Yanga, Nassredine Nabi aliamua kumuondoa Saido Ntibanzonkiza eneo hilo na kumchezesha Fei na bado aliendelea kumpa kile anachokihitaji na aliwahi mwenyewe kukaririwa na Mwanaspoti akisema: “Ni ngumu kuwa na Feisal dhidi ya Saido halafu ukamuweka nje. Huyu ni kijana na anaweza kucheza dakika zote 90 vizuri akiwa uwanjani na akafanya kile unachotaka.”
Fei (23), alijiunga na Yanga Agosti 15, 2018 akitokea JKU ya Zanzibar, huku Jangwani wakifanya umafia wa kumpora mikononi mwa Singida United waliokuwa wameshampa mkataba mkononi na tangu ajiunge amekuwa mmoja wa mihimili ya timu hiyo na Taifa Stars na katika Ligi Kuu ya msimu huu ameshatupia mabao mawili kupitia mechi tatu (kabla ya mechi za jana).