Home news HIZI HAPA DAKIKA 360 ZA JASHO NA DAMU KWA KOCHA MPYA SIMBA…AKISHINDWA...

HIZI HAPA DAKIKA 360 ZA JASHO NA DAMU KWA KOCHA MPYA SIMBA…AKISHINDWA HUENDA AKAFUKUZWA…


MASHABIKI wa Simba kwa sasa wanahesabu saa tu kabla ya klabu yao kutambulishwa rasmi kocha mkuu wao mpya, Pablo Franco Martin kutoka Hispania, lakini kocha huyo wa zamani wa Getafe na Al Qadsia ya Kuwait, ameingia kwenye mtego mgumu kutoka kwa vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga. Anatoboa, hatoboi?

Mabosi wa Simba wapo hatua ya mwisho kabla ya kumtambulisha Pablo kuanzia leo ili kuchukua nafasi iliyoachwa na Mfaransa Didier Gomes tayari kwa maandalizi ya mechi nne ngumu zikiwamo mbili za Ligi Kuu na nyingine za kimataifa kabla ya kuvaana na vijana wa Nasreddine Nabi, Yanga.

Simba inatarajiwa kuikaribisha Yanga kwenye Kariakoo Derby itakayopigwa Desemba 11 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, likiwa ni pambano la 107 kwa timu hizo kukutana katika Ligi ya Bara tangu mwaka 1965.

Pambano hilo litakuwa la tano katika Ligi Kuu tangu mwaka 2020, huku Simba ikiwa haijawahi kuonja ushindi wowote, kwani ilipasuka mara mbili ikiwamo mechi yao ya mwisho iliyopigwa Julai 7 baada ya awali kuahirishwa kitatanishi Mei 8 na nyingine mbili ziliisha kwa sare.

Kwa namna ilivyo ni wazi kocha huyo mpya atakuwa na kibarua kigumu mbele ya Kocha Nabi wa Yanga ambaye miezi michache iliyopita alikiongoza kikosi chake kupata ushindi wa mechi sita tofauti za mashindano zikiwamo tano za ligi na moja ya Ngao ya Jamii wakiitungua Simba kwa bao 1-0.

Pablo atakuwa na kazi kubwa kwanza ya kuhakikisha anafanya vema kwenye mechi zake nne za awali kabla ya kuvaana na Yanga Desemba 11, huku akilazimika pia kuifanya timu yake icheze soka tamu la pasi nyingi na kushambulia kama nyuki ili kuzima kelele za wanayanga wanaotambia timu yao.

Kwa msimu huu, Yanga imekuwa ikisifika kwa kupiga pira biriani lenye pasi nyingi na kuwatia presha wapinzani wao, jambo lililoifanya ikae kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ikiwa ndio timu pekee iliyoshinda mechi zake kwa asilimia zote (100%) na kufunga mabao mengi ikitupia tisa hadi sasa.

DK 360 ZA KIBABE

Kabla ya pambano hilo la Yanga litakalomaliza ubishi baina ya timu hizo kwa msimu huu, kocha huyo mpya wa Simba atakuwa na dakika 360 za kibabe ili kudhihirisha anaiweza kazi, kwanza ni kushinda mechi zake za Ligi ili kupunguza pengo la pointi baina ya timu yake na vinara Yanga.

Kwa sasa timu hizo zimetenganishwa kwa tofauti na pointi nne, Simba ikiwa na 11 na watani wao 15, huku kama akitambulishwa siku hizi mbili za mwanzoni mwa wiki hii ataanza kukinoa kikosi kikiwa na nyota wachache kwani wengine wapo kwenye timu zao za taifa zinazocheza katikati ya wiki.

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUWA 'MDEBWEDO' TENA MSIMU HUU...KIFARU WA MTIBWA SUGAR AVUNJA UKIMYA...AFUNGUKA HAYA...

Nyota wake wengine watarejea siku chache kabla Pablo hajaanza kibarua cha kuiongoza timu hiyo kwenye mechi yake ya kwanza ya Ligi dhidi ya Ruvu Shooting ‘Wazee wa Kupapasa’ itakayopigwa jijini Mwanza.

Mechi hiyo itapigwa Novemba 19 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, huku wapinzani wao ambao ndio wenyeji wa mchezo huo wakiwa na rekodi nzuri ya mechi ya kwanza ya msimu uliopita walipoitungua Simba bao 1-0, siku chache baada ya kupasuliwa na Tanzania Prisons mjini Sumbawanga.

Baada ya kumalizana na dakika 90 za awali, Pablo atarudi jijini Dar es Salaam kuiongoza Simba dhidi ya Red Arrows ya Zambia katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika kuwania kutinga makundi, mechi itakayopigwa Novemba 28 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mara ya mwisho Simba kucheza dhidi ya timu ya Zambia katika mechi za kimataifa ilikuwa Desemba 23, 2018 katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nkana FC na kushinda mabao 3-1 yaliyowavusha kuingia makundi baada ya awali kucharazwa ugenini 2-1.

Mara baada ya kumalizana na Wazambia jijini Dar es Salaam siku chache baadaye Simba itawaalika Geita Gold katika mechi nyingine ya Ligi itakayopigwa Desemba Mosi kisha Pablo atasafiri na timu hiyo hadi Zambia kurudiana na maafande wa anga, Red Arrows ili kuamua hatma yao itinge makundi au iungane na Yanga, Azam na Biashara United zilizotolewa mapema katika michuano ya CAF msimu huu.

Mechi hiyo ya marudiano ya Simba dhidi ya Wazambia itapigwa Desemba 5, siku sita tu kabla ya pambano lao la watani, ambalo hata hivyo halitabiriki kwani halichelewi kuahirishwa na mamlaka kama ilivyowahi kutokea kwenye mechi kadhaa za watani hao zikiwamo zote mbili za msimu uliopita.

Rekodi zinaonyesha mara ya mwisho Simba kucheza Zambia ilikuwa Desemba 16, 2018 ilipokubali kichapo cha mabao 2-1 mbele ya Nkana mjini Kitwe.

Kama Pablo na wasaidizi wake watatoboa kwenye mechi hizo nne ngumu kisha kuja kuikalisha Yanga ni wazi atawarejeshea furaha wana Msimbazi ambao kwa sasa wamekuwa wanyonge kwa jinsi watani wao wanavyoupiga mwingi na kupata matokeo mazuri uwanjani kulinganisha na wao.