KIKOSI cha Azam FC kimerejea kambini kuanza maandalizi makali ya mchezo ujao dhidi ya KMC utakaopigwa Novemba 21 saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Uhuru.
Wachezaji wa Azam mchezo wao wa mwisho dhidi ya Geita walishinda bao 1-0 lililofungwa na Rogers Kola.
Akizungumza hivi karibuni, kocha msaidizi wa timu hiyo, Bahati Vivier alisema wameanza kujiandaa na mechi yao ijayo na jambo zuri wachezaji wote ambao hawana majeraha na hawakuitwa katika timu za Taifa tayari wameshajiunga katika mazoezi.
“Tunajiandaa na mechi dhidi ya KMC na tayari baada ya wachezaji kuwasili tuliwapima miili yao kwa kuwakimbiza ili kujua wana utimamu kwa kiasi gani baada ya kukaa nyumbani kwa siku mbili tatu,” alisema.
“Tutafanya mazoezi ya nguvu katika pande zote kuanzia ulinzi mpaka ushambuliaji kuhakikisha tunakuwa bora kwenye mechi zetu zinazokuja baada ya majukumu ya timu ya Taifa kumalizika.”
Azam wanashika nafasi ya nane wakiwa na pointi saba huku KMC wakishika nafasi ya 15 na pointi mbili na wote wakicheza mechi tanotano.