KIUNGO mkabaji Mkongomani wa Yanga, Mukoko Tonombe ni kati ya wachezaji huru katika kikosi hicho wanaoruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine.
Huyo ni mchezaji wa pili katika kikosi hicho cha Mtunisia, Nasreddine Nabi mwingine ni mshambuliaji Ditram Nchimbi ambaye amejitoa katika kikosi hicho.
Kiungo huyo hivi sasa amekosa nafasi ya kudumu katika kikosi hicho tangu kuanza kwa msimu huu ambao una viungo wengi bora akiwemo Khalid Aucho na Yannick Bangala.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mkurugenzi Uwekezaji na Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya timu hiyo, Injinia Hersi Said alisema Mukoko amebakisha miezi sita katika mkataba wake.
Said alisema kiungo huyo alisaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu katika msimu uliopita na usajili wa dirisha dogo Januari ndiyo mkataba wake unamalizika.
Aliongeza kuwa aliyekuwa kiungo wao mshambuliaji, Tuisila Kisinda yeye alisaini mkataba wa miaka miwili kabla ya kumuuza kwenda klabu ya Berkane ya nchini Morocco.
“Kati ya kazi zenye ugumu ni usajili wa wachezaji.“Kati ya wachezaji tuliopata nao ugumu basi ni akina Mukoko na Tuisila, kwani ili utoke na mchezaji nchini hapo lazima uwe na kibali maalum na ukikutwa naye Uwanja wa Ndege wa kwao na huna kibali, basi ujue una kesi.
“Usajili wa Mukoko ulikuwa wa mwaka mmoja na miezi ambao unamalizika Januari, mwaka huu na hivyo anaruhusiwa kufanya mazungumzo sasa na Kisinda yeye alisaini miaka miwili,” alisema Said.