Home news BALAA JIPYA YANGA HILI HAPA…KAZE AFUNGUKA KILA KITU…MAYELE , ‘FEI TOTO’ WATAJWA…

BALAA JIPYA YANGA HILI HAPA…KAZE AFUNGUKA KILA KITU…MAYELE , ‘FEI TOTO’ WATAJWA…


WANANCHI huko mtaani hawapoi wala hawaboi kutokana na tambo zao kibao kulingana na ubora wa timu yao ya Yanga kuendelea kuwapa mautamu inapokuwa uwanjani.

Yote hayo ni kutokana na soka safi wanalopiga wachezaji wa chama hilo na hadi sasa ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kucheza mechi tano na kushinda zote ikikusanya alama 15, ikifunga jumla ya mabao tisa na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja tu.

Maufundi hayo yanachagizwa na ubora wa benchi la ufundi chini ya kocha mkuu Mtunisia, Nasreddine Nabi akishirikiana na kocha msaidizi Cedric Kaze raia wa Burundi.

Gazeti la Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Kaze kwa niaba ya benchi la ufundi na kufunguka kila kitu huku akieleza chanzo cha soka safi na ubora wa kikosi kile cha wanajangwani kuwa ni safu ya ushambuliaji.

Kaze amefunguka kuwa kwa sasa nguzo kubwa ya Yanga ni eneo la ulinzi kwa maana ya mabeki wa kati Dickson Job na Bakari Mwamnyeto sambamba na kipa Djigui Diarra wakishilikiana na wachezaji wengine ambao wanajenga falsafa mpya ya kucheza pasi nyingi.

Kocha huyo ambaye pia huwa anatumia muda mwingi kuwasoma makocha wenye mafanikio makubwa duniani akiwemo Pep Guadiola wa Manchester City na Jurgen Klopp wa Liverpool ameeleza kuwa wako kimkakati na wanaendelea kufanya kazi ya ziada ili kuboresha falsafa hiyo mpya.

“Katika mpira wa kisasa ili mtu aweze kuingiza falsafa mpya ya kucheza mpira wa chini na kuanza kucheza kutokea nyuma inahitaji kazi kubwa sana na tunaendelea kuifanyia kazi,” alisema Kaze na kuongeza;

Katika falsafa yetu kipa na beki ndio mhimili mkuu wa timu kwani mara nyingi hupata mpira bila kubugudhiwa zaidi na kwa aina hii tunayocheza sasa inahitaji mabeki bora wa kati na mwenye akili na ujuzi zaidi maana ndio wanaanzisha mashambulizi,” alisema kaze na kuendelea kueleza namna Yanga inavyofanikiwa na kutoa burudani;

Ndio maana timu yetu (Yanga) ikiwa inacheza unawaona Job na Mwamnyeto wakicheza kwa utulivu na kupigiana pasi nyingi pamoja na kipa na kuanzisha mashambulizi kwa viungo kisha kuomba tena mpira kwani wao ndio wataamua timu ichezeje,” alisema Kaze.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA SPOTI XTRA ALHAMISI

AWATAJA MAYELE, FEISAL

Kaze alifunguka kuwa kwa mfumo wa sasa wa Yanga yupo radhi amuache mshambuliaji mwenye ubora na maufundi kibao ila awe na beki mtulivu, mwenye kontroo na akili kama ilivyo kwa Job.

“Hii tuliianza msimu uliopita tukampata Job ambaye ana sifa zote hizo na msimu huu tumemuongeza Diarra ndio maana unaona tunaimarika na kucheza vizuri,” alisema Kaze na kuongeza;

“Kule mbele tuna wachezaji bora na mafundi akiwemo Fiston Mayele na Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambao wanaongeza ubora wa timu sambamba na viungo wetu lakini yote hayo huanzia kwa mabeki.

Mtu kama Feisal anapata mipira mingi lakini anakutana na wapinzani wengi ambao humkaba na kumbugudhi hivyo inatubidi tujenge ukuta bora kwanza ambao kila shambulizi litaanzia kwao kisha kuwafikia wachezaji wengine kirahisi zaidi kuliko kuwapa shida,” alisema Kaze.