Home news KISA KUKOSA NAMBA KIKOSI CHA KWANZA YANGA…MAKAMBO ALIA NA UONGOZI…AKASIRIKA KUTOPANGWA…

KISA KUKOSA NAMBA KIKOSI CHA KWANZA YANGA…MAKAMBO ALIA NA UONGOZI…AKASIRIKA KUTOPANGWA…


STAA wa mashabiki wa Yanga, Heritier Makambo amekiri kwamba hali ya kukaa benchi au jukwaani aliyokutana nayo ndani ya kikosi cha sasa hakuitegemea.

Mchezaji huyo ambaye alikuwa amebeba mategemeo makubwa kwa mashabiki amesema kwamba amelazimika kukaa na kocha na uongozi wakati huu ambao ligi imesimama ili kujua kiundani kwamba anakwama wapi na afanye nini.

Ameweka wazi kwamba hali aliyokumbana nayo katika siku za hivi karibuni licha ya kwamba ni ya kawaida kwenye soka lakini yeye imemfanya kuwa mnyonge.

Makambo moja ya wachezaji waliotikisa usajili wa Yanga na kuwapa matumaini kibao Wanajangwani waliokuwa wamekosa furaha na timu hiyo baada ya kutofanya vizuri msimu uliopita lakini mambo yamemuendea kombo.

Makambo alisema jambo hilo limetokana na kushindwa kupata nafasi ya kucheza kama ambavyo alitarajia hapo awali wakati anasajiliwa na alivyocheza vizuri mechi ya Zanaco akifunga bao na kukumbushia staili yake ya kuwajaza.

Alikiri kuna kipindi alikuwa anapewa baadhi ya mazoezi lakini alishindwa kufanya vizuri kutokana na akili yake kutokuwa mchezoni.

“Ligi iliposimama nimepata nafasi ya kuongea na kocha pamoja na viongozi na kuna mambo tumezungumza ambayo rasmi yamenirudisha akili yangu katika soka na kufanya kile ambacho kinahitajika,” alisema Makambo ambaye ni raia wa DR Congo na kuongeza;

“Nimeanza mazoezi yangu binafsi katika wakati huu kabla ya yale ya timu ili kuimarika zaidi na tutakapokwenda mazoezini nitafanya vitu vilivyokuwa bora kwa kutimiza majukumu yangu pengine zaidi ya wakati wote,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine Makambo aliongezea kikosi cha Yanga msimu huu kina wachezaji wengi wazuri ambao ukiangalia katika kila eneo kuna ushindani wa kutosha.

Makambo alisema Yanga ambayo alicheza awamu ya kwanza haikuwa bora kama ya wakati huu na aliweza kuibuka mfungaji bora wa kikosi, akiamini kama atacheza sasa atafunga zaidi ya idadi ile.

“Nimerudi mchezoni naendelea kufanya kila kilicho bora katika mazoezi ili kumshawishi kocha kunipa nafasi ya kucheza na ikitokea nikapata muda wa kutosha uwanjani nitafunga zaidi,” alisema Makambo na kuongeza;

SOMA NA HII  KIUNGO YANGA SC ATIMKIA ZAKE LIBYA...ISHU NZIMA IKO HIVI....

“Benchi la ufundi lenyewe ndio lenye uamuzi wa mwisho kunitumia au vinginevyo, lakini nakwenda kuonyesha kiwango bora na kutimiza majukumu yangu ya kufunga mabao ili kuwapa Wananchi kile ambacho wanahitaji kukiona kutoka kwangu,” alisema

KIWANGO CHA MAYELE

Kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga straika ambaye anaanza ni Mkongomani mwingine, Fiston Mayele ambaye mpaka sasa katika Ligi Kuu Bara ameweka mabao mawili kambani.

Makambo alisema anafahamu uwezo alionao Mayele tangu wakiwa DR Congo. “Ubora wake ni sehemu ya ushindani kwangu.

“Naheshimu viwango vya wachezaji wengine ambao hutumika katika nafasi ambayo nacheza kwani huo ndio ushindani ambao unahitajika kwa timu ambayo inahitaji kufanya vizuri.”

Katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Azam pamoja na Ruvu Shooting Makambo hakuwa katika orodha ya wachezaji 20, ambao walivaa jezi kwa ajili ya kutumika kwenye michezo hiyo.

Makambo alisema halikuwa jambo zuri kwake kutokana na uwezo ambao anaamini anao hawezi kushindwa kuwemo katika wachezaji 20, lakini pengine kocha hakuridhika naye ndio maana alimuacha jukwaani.

“Nafahamu katika mechi moja wachezaji wa kigeni tunatakiwa kuwa nane lakini ubora nilionao nina imani kubwa nastahili kuwepo kati yao,” alisema Makambo na kuongeza;

“Nitaendelea kupambana mpaka dakika ya mwisho ili kutimiza malengo ya timu pamoja na yale yangu binafsi sitakubali kuona kuna changamoto inanikwamisha.”