Home news USAJILI DIRISHA DOGO WAGAWA MASTAA SIMBA…AJIB, WAWA, MUGALU NA KIBU DENIS WATAJWA…

USAJILI DIRISHA DOGO WAGAWA MASTAA SIMBA…AJIB, WAWA, MUGALU NA KIBU DENIS WATAJWA…


WAKATI hekaheka za usajili wa dirisha dogo msimu huu zikielekea kuanza, nyota wa zamani wa Simba wamekuwa na mtazamo tofauti wa usajili huo kwenye kikosi chao.

Baadhi ya nyota hao wanaamini Simba inahitaji kusajili mshambuliaji na beki ambaye atachukua nafasi ya Serge Wawa, ingawa wengine wamesisitiza hawaoni sababu za timu hiyo kuingiza wachezaji wapya kwenye dirisha dogo.

Kauli za wachezaji hao imekuja kutokana na kuwepo kwa mjadala juu ya ubora wa washambuliaji wa timu hiyo na kiwango kizima cha Simba tangu kuanza msimu huu na aina ya wachezaji iliyonao.

Ingawa uamuzi wa kuongeza wachezaji au vinginevyo uko chini ya Kocha Pablo Franco, magwiji hao wametofautiana kuhusu ingizo jipya wakati wa dirisha dogo.

“Sioni sababu ya Simba kuongeza wachezaji kwenye dirisha dogo, hawa waliopo wanatosha,” alisema Fikiri Magosso, kauli sawa na iliyotolewa na Lubigisa Madatta.

Hata hivyo, Malota Soma na Moses Mkandawile wametofautiana na mtazamo huo wakiamini Simba inahitaji kuongeza wachezaji wawili katika nafasi ya ushambuliaji na beki wakati wa dirisha dogo.

“Washambuliaji wetu ni kama homa za vipindi, kuna wakati zinapanda na kuna wakati zinashuka, Bocco (John), binafsi namuona bado yuko vizuri ingawa kwa sasa ana changamoto ya kukosa mabao, Kibu (Denis) changamoto yake ni kutokuwa makini golini, kama ikitokea Mugalu kaumia au Lwanga inakuwa changamoto.

“Kagere ni mpambanaji, lakini kwa sasa anachezea uzoefu na si mchezaji wa kumtegemea kumtumia miaka mitatu ijayo, Simba inahitaji ‘damu’ changa pale mbele,” alisema Malota.

Mkandawile pia alisema timu hiyo inahitaji kupata mtu mbunifu wa mwisho katika ufungaji, lakini pia kuwa na beki ambaye atamsaidia Wawa.

“Kuna Kennedy Juma ni beki mzuri, ila sijui ni kwanini hapati nafasi ya kucheza, ila ni mchezaji ambaye binafsi naamini viatu vya Wawa kwenye kikosi cha Simba vinamtosha,” alisema.

Magosso anaamini usajili wa Simba dirisha dogo utegemee na majeraha ya Mugalu.

“Sioni kama Simba inahitaji kufanya usajili wakati wa dirisha dogo, labda mahitaji hayo yaangalie na majeraha ya Mugalu, kocha Pablo watu anao ni namna tu ya kuwatumia.

SOMA NA HII  UTAMU WA LIGI YA MABINGWA HUU HAPA NA MERIDIAN BET

“Mfano Kennedy Juma, apewe nafasi ya kucheza ni beki bora sana lakini hapewi nafasi,” alisema Magosso.

Lubigisa hakutofautiana na Magosso na kusisitiza timu hiyo kama itafanya usajili kwenye dirisha dogo basi ni wa presha tu, lakini wachezaji waliopo wanajitosheleza.

“Ajibu (Ibrahim) anatakiwa kupambana, asiwe mchezaji wa mechi mbili kisha anapotea, lakini Dilunga wa mwaka jana sio wa sasa, Mkude pia amerudishwa binafsi nakiona kikosi cha Simba kiko vizuri, wakiamua kuongeza watu dirisha dogo basi ni kwa shoo tu,” alisema.

Kuhusu kiwango ambacho Simba imekionyesha kwenye mechi tano za Ligi mpaka sasa, Lubigisa alisema ni kizuri na kinachoonekana sasa ni presha tu.

“Hata msimu uliokwisha tulianza kama msimu huu tu, hivyo kinachoonekana sasa ni presha tu ila Simba iko vizuri,” alisema.

Katika mechi tano, Simba imeshinda tatu, imefungwa moja na kutoka sare moja ikiwa nafasi ya pili.