WAKATI Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limefunga rasmi dirisha dogo la usajili, Klabu ya Simba imesema itafanya usajili wa kurekebisha kikosi chake kwa kuzingatia mwongozo utakaotolewa na Kocha Mkuu, Pablo Franco pamoja na benchi lake la ufundi.
Tayari tetesi zinasema nyota Moses Phiri kutoka Zambia ametua nchini kwa ajili ya kukamilisha mchakato wa kujiunga na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, amesema katika kipindi hiki wamepanga kujiimarisha kwa sababu wanahitaji kuona wanaendelea kufanya vizuri kwenye michuano mbalimbali wanayoshiriki.
“Tutafanya usajili wa kuboresha kikosi chetu, lakini hii itategemea na matakwa ya mwalimu wetu na benchi la ufundi, wao ndiyo watatuambia sehemu gani ina mapungufu na sisi tutawatekelezea,” alisema Mangungu.
Simba ndiyo timu pekee iliyobaki kwenye mashindano ya kimataifa, ambapo wadau wa soka wameshauri kikosi hicho kinahitaji maboresho katika baadhi ya idara zake ikiwamo safu ya kiungo mshambuliaji ambaye atakuwa na uwezo kuichezesha timu.
TFF ilitoa taarifa ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili kwa ajili ya Ligi Kuu, Ligi ya Championiship, First League na Ligi Kuu ya Wanawake na dirisha hilo litafungwa ifikapo Januari 15, mwakani.
Shirikisho hilo pia limezitaka klabu zote kuheshimu kalenda hiyo iliyotolewa na watakaokuwa na changamoto yoyote wawasiliane na Idara ya Mashindano kwa ajili ya kupata ufumbuzi.