Aliyewahi kuwa Nahodha na Beki wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Boniface Pawasa anaamini wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (Simba SC) wamepata Ganda la Ndizi kwenye michuano hiyo.
Pawasa ametoa kauli hiyo, kufuatia Shirikisho la Soka Barani Afrika kupanga Makundi ya Kombe la Shirikisho jana Jumanne (Desemba 28) mjini Cairo, Misri.
Simba SC imepangwa Kundi D sambamba na US Gendarmerie ya Niger, RS Berkane ya Morocco na Asec Mimosa ya Ivory Coast.
Pawasa ambaye kwa sasa ni Kocha wa timu ya taifa ya Soka la Ufukweni amesema: Kwa ufupi naweza kusema kundi lao ni jepesi. Uzoefu wao ni mkubwa tofauti na timu zingine na kwangu mimi naona timu tishio ni ASEC Mimosas kutokana na kukaa kwao nje ya mashindano haya kwa muda mrefu.
Simba SC itaanzia nyumbani Februari 13 kwa kuikaribisha Asec Mimosa ya Ivory Coast, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kisha itakwenda ugenini Niger kupambana na US Gendarmerie Februari 20 na Februari 27 itasafiri kuelekea Morocco kupambana na RS Berkane.
Machi 13 Simba SC itarejea Dar es salaam kucheza dhidi ya RS Berkane Uwanja wa Benjamin Mkapa huku mchezo unaofuata itacheza dhidi ya Asec Mimosa ugenini Machi 20 kabla ya kumaliza michezo ya hatua ya makundi kwa kuikaribisha US Gendarmerie Aprili 03.