WAKATI mkataba wake ukielekea ukingoni, nyota wa Yanga, Mrundi, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ amezuiwa kuondoka na mabosi wa timu hiyo na kumtaka wakae chini kujadili kuongezewa mkataba wa kuendelea kukitumikia kikosi hicho.
Saido ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu, amekuwa na kiwango kizuri msimu huu ambapo tayari amefunga mabao matatu kwenye Ligi Kuu Bara.
Mtu wa karibu na nyota huyo fundi wa mipira iliyokufa ikiwemofaulo na penalti, ameliambia amesema kuwa: “Ntibazonkiza anamaliza mkataba na Yanga mwishoni mwa msimu huu na mpaka sasa hajasaini mkataba mpya.
“Viongozi waliposikia kuwa ana mpango wa kuondoka baada ya kupata ofa Uarabuni, wakaamua kukaa naye kikao ila inaonekana kama anataka fedha nyingi ambazo Yanga hawawezi kuzitoa.
“Baada ya mazungumzo ya kwanza kushindikana, ndipo GSM (Gharib Said Mohamed, mdhamini wa Klabu ya Yanga) akamtafuta na kutaka amsubiri mpaka arejee nchini ili waweze kukaa na kuzungumza kuhusu suala hilo.
“Kila mtu anaona kiwango chake ndiyo maana hata hizo timu zikamtafuta na kama Yanga hawatampa mkataba mapema basi anaweza kuondoka maana ofa za Uarabuni huwa ni kubwa sana.”
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, alisema: “Kwa sasa nipo bize, nitafute baadaye.” Alipotafutwa baadaye hakupatikana.